Thursday, June 18, 2015
RAIS KIKWETE AKUNWA NA UTITIRI WA WAGOMBEA URAIS NDANI YA CCM.
Do you like this story?
RAIS
Jakaya Kikwete ameelezea kufurahishwa na wingi wa wagombea waliojitokeza kuomba
ridhaa ya kuteuliwa kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, akisema ni
jambo zuri na ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka katika chama
hicho.
Aidha,
amesema pia msururu wa wagombea hao ambao sasa wamefikia 36, ni uthibitisho
kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio na
kwamba kinyume cha hapo, wengi wasingependa kujihusisha nacho.
Pamoja
na kufurahishwa huko, ameendelea kusisitiza kuwa, yeye binafsi hana mgombea
urais anayempendelea kwa sababu wagombea wote ni wa kwake na wa chama chake,
isipokuwa anayo kura moja tu ambayo ataitumia mwezi ujao wakati wa vikao
mbalimbali kuamua nani awe mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Rais
Kikwete amesema hayo usiku wa kuamkia juzi mjini Johannesburg, Afrika Kusini
wakati akizungumza na Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza
Kitengo cha Masuala ya Afrika, Linda Thomas- Greenfield.
Viongozi
hao wawili walikuwa wanahudhuria Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Nchi Wanachama wa
Umoja wa Afrika kwenye Kituo cha Mikutano cha Sandton Covention Centre,
Johannesburg, Afrika Kusini uliomalizika jana.
Mwanzoni
tu mwa mazungumzo hayo, Linda alimwuliza Rais Kikwete: “Mheshimiwa Rais, je
unaye mgombea yeyote ambaye unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea?”
Rais
Kikwete alimjibu: “Sina mgombea ninayempendelea, wagombea wote ni wa kwangu, ni
wa Chama changu, isipokuwa ninayo kura moja ambayo kwa mujibu wa taratibu za
haki katika Chama chetu nitaitumia katika vikao mbalimbali.”
Kuhusu
kile kinachoitwa utitiri wa wagombea, Rais Kikwete alisema wingi wa wagombea ni
jambo zuri kwa CCM. “Hiki ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya kujadili
kwa nafasi nani awe mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea wengi zamu hii kwa
sababu ya wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka katika nchi yetu katika miaka ya
karibuni. Vile vile, wingi wa wagombea unathibitisha mafanikio yetu katika
miaka 10 iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu wangeogopa kujitokeza kugombea
nafasi hiyo.”
Aidha,
Rais Kikwete alisema hana tatizo na kujitokeza kwa wagombea wengi wa nafasi ya urais
zamu hii kupitia CCM kwa sababu huwezi kuwazuia watu kugombea nafasi hiyo kwa
sababu ni haki yao.
Alisisitiza
wingi wa wagombea zamu hii ni jambo zuri na ni ushahidi wa kiasi cha uhuru
ambao umejengeka katika chama hicho na uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania
katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS KIKWETE AKUNWA NA UTITIRI WA WAGOMBEA URAIS NDANI YA CCM.”
Post a Comment