Thursday, June 4, 2015
WITO UMETOLEWA KWA WAMILIKI WA VIWANDA KUENDELEA KUTOA USHIRIKIANO KWA WADADISI WANAOKUSANYA TAARIFA ZA SENSA YA VIWANDA NCHINI
Do you like this story?
Wito umetolewa kwa wamiliki wote wa viwanda
kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wasimamizi na wadadisi wanaokusanya taarifa za
Sensa ya Viwanda inayoendelea hapa nchini.
Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Viwanda
na Biashara Mhe. Dkt. Abdallah Kigoda wakati akizungumza na waandishi wa habari
mkoani Dododoma ambapo amesema ukusanyaji taarifa kwa nchi nzima umefikia
wastani wa asilimia 80.5.
"Hadi kufikia tarehe 24 Mei, 2015 jumla
ya viwanda vidogo 9,540 sawa na asilimia 82 pamoja na viwanda vya kati na
vikubwa 1,158 sawa na asilimia 79 vilikamilika kukusanywa taarifa zake. Hii
inafanya ukusanyaji Takwimu kwa nchi nzima kuwa wastani wa asilimia 80.5",
amesema Dkt. Kigoda.
Aidha, Waziri Kigoda amesema licha ya
mafaniko hayo, bado kuna kazi kubwa ya kukamilisha viwanda vilivyobaki ambavyo
ni takriban 2,032 sawa na wastani wa asilimia 19.5.
"Hivyo, nawaasa wamiliki wote wa viwanda
hususani katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Morogoro, Tabora, Kigoma
na Manyara kutoa ushirikiano zaidi na wa kutosha kwa zoezi hili ili ifikapo
mwisho wa mwezi huu wa Juni, 2015, tuweze kuhitimisha", amesisitiza Dkt.
Kigoda.
Waziri Abdallah Kigoda amesema lengo kuu la
Sensa ya Viwanda ni kukusanya takwimu sahihi zinazohusu Sekta ya Viwanda nchini
ambazo zitawezesha kupata viashiria sahihi vya uchumi pamoja na taarifa muhimu
za viwanda kama vile orodha ya viwanda kimkoa, anuani na mahali vilipo, aina ya
umiliki na utaifa wa wamiliki.
Taarifa nyingine ni pamoja na mwaka
ambao viwanda hivyo vimeanza uzalishaji, shughuli kuu ya viwanda husika, idadi
ya wafanyakazi, gharama za malipo mbalimbali kwa wafanyakazi, mapato
yanayotokana na uzalishaji na gharama za uzalishaji.
Lengo lingine la Sensa ya Viwanda ni kupima
na kufuatilia mabadiliko yanayotokea katika Sekta ya Viwanda ili kuiwezesha
Serikali kuboresha sera na programu za kukuza ajira, kupanga na kufuatilia
utekelezaji wa mipango ya maendeleo kama vile Malengo ya Milenia, Dira ya
Maendeleo ya Tanzania, 2025, Malengo ya MKUKUTA na Mpango wa Taifa wa Matokeo
Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN).
Jumla ya Wadadisi 198 wameajiriwa kwa ajili
ya kufanya kazi ya kukusanya Takwimu na taarifa viwandani ambapo wanasimamiwa
na Mameja Takwimu wa Mikoa, Watakwimu kutoka Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya
Takwimu na Maafisa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WITO UMETOLEWA KWA WAMILIKI WA VIWANDA KUENDELEA KUTOA USHIRIKIANO KWA WADADISI WANAOKUSANYA TAARIFA ZA SENSA YA VIWANDA NCHINI”
Post a Comment