Thursday, June 4, 2015

SIMBA YAAMUA KUMPELEKA MESSI POLISI


Msemaji wa Simba, Hajji Manara


Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
UONGOZI wa Simba umesema umeamua kulifikisha polisi sakata la usajili wa kiungo mshambuliaji Ramadhani Singano 'Messi' ili kulinda taswira ya klabu hiyo.

Messi anadai kutotambua uhalali wa mkataba wake wa miaka mitatu na Simba uliopo katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) huku akisisitiza ana mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo ya Msimbazi utakaomalizika Julai Mosi mwaka huu.

Hajji Manara, msemaji wa Simba, katika mahojiano na moja ya vituo vya redio jijini hapa leo, amesema kuwa kutokana na mvutano ulioibuka baina ya pande zote mbili, klabu imeona ni vyema kulifikisha suala hilo mbele ya vyombo vya dola ili lipatiwe ufumbuzi.

"Simba ni taasisi kubwa, suala hili linachafua 'image' (taswira) ya taasisi hii. Tukumbuke pia kwamba Simba ina wadhamini. Inaposdemwa kwamba tumeghushi nyaraka likiwamo dole gumba la Messi, ni kashfa kubwa. Wadhamini wanatuelewaje?" Amehoji Manara bila kutaja lini hasa suala hilo litatinga polisi.

Wakati Simba wakitishia kulifikisha suala hilo mikononi mwa polisi, tayari Chama cha Wachezaji wa Soka Tanzania (Sputanza) kimeshalifikisha sakata hilo mikononi mwa TFF ili litatuliwe na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho hilo.

Mwenyekiti wa Sputanza, Mussa Kisoky, alisema jijini jana kuwa walifikia hatua ya kuonana na uongozi wa TFF baada ya kupewa maelezo na winga huyo mwenye umri wa miaka 21.

0 Responses to “SIMBA YAAMUA KUMPELEKA MESSI POLISI”

Post a Comment

More to Read