Friday, September 25, 2015
RAIS KIKWETE ASEMA HASHANGAI SERIKALI YAKE KUKOSOLEWA NA MAGUFULI.
Do you like this story?
RAIS Jakaya Kikwete, amesema
hamshangai mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.John Magufuli kwa
kukosoa utendaji kazi wa Serikali yake katika mikutano yake ya kampeni
inayoendelea.
Rais Kikwete, alitoa kauli hiyo
juzi, wakati akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya NDI yenye uhusiano na
Chama cha Democratic, IRI yenye uhusiano na Chama cha Republican, IFES na
United States Institute of Peace (USIP) mjini Washington nchini Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya
Mawasiliano Ikulu mjini Dar es Salaam jana, ilisema Rais Kikwete anaunga mkono
mwenendo wa kauli za Dk. Magufuli kwa sababu kila kiongozi anapoingia
madarakani anakuwa na aina yake ya uongozi.
“Wamepata kuja watu kwangu,wakaniambia
mgombea wetu wa CCM anashutumu na kusahihisha Serikali yangu na utendaji wake
kwenye mikutano ya kampeni. Niliwaambia hivi anavyofanya mgombea wetu ni
jambo sahihi kabisa,lazima afanye hivyo.
“Niliwaambia nchi yetu, inahitaji
mawazo mapya na mwelekeo mpya ulio tofauti na uongozi wangu. Niliwaambia
tusiporuhusu jambo hilo kufanyika, nchi yetu itabakia pale pale ambako
nimeifikisha mimi.
“Haya yatakuwa na makosa makubwa kwa
sababu nchi yetu lazima isonge mbele kwa mawazo mapya,uongozi na staili mpya ya
uongozi.
“Haya ndiyo anayosema mgombea wetu.
Vinginevyo ni jambo lisilokuwa na maana kubadilisha uongozi kama hatuko tayari
kukubali, kila kiongozi lazima awe na staili yake ya uongozi na namna ya
kuongoza na kuendesha nchi yetu,” alisema.
Katika mikutano yake Dk. Magufuli
amekuwa akieleza namna asivyoridhishwa na uwepo wa huduma mbovu katika sekta
mbalimbali ikiwamo afya na maji, hali inayowafanya wananchi waendelee
kutaabika.
Dk. Magufuli amekuwa akishangaa
kuona dawa zinakosekana katika hospitali za Serikali huku dawa hizo
zikipatikana katika maduka binafsi na kuahidi kupambana na majizi na mafisadi.
Mgombea huyo pia amekuwa akishangaa
pale ambapo baadhi ya watumishi wanapoharibu aidha kwa kuiba fedha za umma au
uzembe kazini kuhamishwa vituo vya kazi, badala ya kufukuzwa na kushitakiwa.
Atamani
kupumzika
Katika hatua nyingine,Rais Kikwete
alisema anatamani muda uende kwa kasi zaidi ili akabidhi madaraka kwa
rais wa awamu ya tano.
“Natamani muda uende nikabidhi
madaraka kwa rais wa tano ili nipate muda wa kumpumzika,baada ya
kazi ngumu ya miaka 10 ambayo ni kama mzigo mkubwa,”alisema Rais Kikwete.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “RAIS KIKWETE ASEMA HASHANGAI SERIKALI YAKE KUKOSOLEWA NA MAGUFULI.”
Post a Comment