Tuesday, October 13, 2015

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI(NEC) YAFYEKA WAPIGA KURA MILIONI MOJA,WALIOJIANDIKISHA WALIKUWA 23,782,558.




Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeyaondoa majina ya wapiga kura zaidi ya milioni moja kutoka katika orodha ya awali ya watu milioni 23.7 waliojiandikisha awali kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR).

Akizungumza kwenye mkutano wa NEC na viongozi wa vyama vya siasa jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema hatua ya kupunguzwa kwa idadi ya wapiga kura inatokana na kukamilika kwa kazi ya uhakiki wa majina ya watu wote waliojiandikisha.

Alisema kuwa awali, idadi ya watu walioandikishwa kupiga kura ilikuwa 23,782,558. 

Hata hivyo, baada ya uhakiki, imebainika kuwa majina 1,031,769 kutoka miongoni mwa orodha ya awali hawastahili kuwamo kwani baadhi yao ni majina ya watu waliojiandikisha zaidi ya mara moja, wengine siyo Watanzania na wapo pia waliokosa sifa nyingine muhimu za kupiga kura, kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kwa sababu hiyo, Jaji Lubuva alisema idadi halisi ya watu watakaokuwa na fursa ya kupiga kura Oktoba 25 ni 22,251,292 kwa Tanzania Bara na wengine 503,193 wa visiwani Zanzibar.

Jaji Lubuva alieleza zaidi kuwa baada ya uhakiki na uchakataji wa taarifa za wapiga kura, NEC ilibaini kuwa wananchi 181,452 walijiandikisha zaidi ya mara moja, huku baadhi yao wakitia fora kwa kujiandikisha hadi mara nane.

Akifafanua zaidi, mwenyekiti huyo wa NEC alisema uhakiki umebaini kuwa wananchi 845,944 waliandikishwa na waandishaji 74,502 waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo kabla ya kuanza uandikishaji, hivyo majina yao yameondolewa, huku majina 3,870 yakibainika kuwa ni ya watu wasiokuwa raia wa Tanzania na hivyo, taarifa zao pia zimefutwa.

VITUO VYA KURA VYAPANGULIWA
Katika hatua nyingine, NEC imetangaza idadi rasmi ya vituo vya kupigia kura nchini kuwa ni 65,105, kati yake 1,580 vikiwa visiwani Zanzibar na vilivyobaki (63,525) vikiwa Tanzania Bara. Idadi hii ni pungufu kulinganisha na idadi ya vituo vilivyokadiriwa awali kabla ya kufanyika kwa uhakiki, ambavyo NEC ilitangaza kuwa vitakuwa 72,000 na kwamba, vinaweza kuongezwa au kupunguzwa kulingana na mahitaji kadiri itakavyoonekana inafaa. Kadhalika, idadi hiyo iliibua shaka pia kutoka kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Mgombea mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, alielezea shaka waliyonayo wiki iliyopita kwa kudai kuwa wastani wa wapiga kura 450 kwa kila kituo unahitaji vituo takribani 53,000 tu kuhudumia wapiga kura milioni 23.7 na siyo 72,000. Duni aliongeza kuwa Ukawa wanahofia kuwapo kwa njama za kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia vituo bandia 20,000 vilivyoongezeka kulingana na mahitaji na uwezo wa kila kituo. 

Hata hivyo, NEC ilipuuza madai hayo kwa kueleza kuwa hakuna vituo vyovyote bandia na kwamba idadi hiyo ni ya makadirio ya awali kabla ya uhakiki.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa jana, Jaji Lubuva alisema kila kituo kinapaswa kuwa na idadi ya wapiga kura kati ya 450 hadi 500, na kwamba ikitokea kuna kituo kinakuwa na wapiga kura zaidi ya 500, watakachofanya ni kukigawanya katika vituo viwili vyenye idadi sawa ya wapiga kura.

“Hiyo ndiyo idadi ya vituo vitakavyotumika siku ya uchaguzi. Isipokuwa wananchi wanapaswa kuhakiki taarifa zao siku nane kabla ya uchaguzi ili kujiepusha na usumbufu utakaotokana na mgawanyo wa vituo,” alisema.

MAJIMBO, KATA 
Lubuva alisema NEC imetekeleza wajibu wake wa kuongeza majimbo mapya 25 na pia Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeanzisha kata mpya 622, hivyo jumla ya majimbo yatakayogombewa kwa nafasi za ubunge ni 264 na kata zote ni 3,957.

Aliongeza kuwa uchaguzi wa wabunge katika majimbo matatu umeahirishwa baada ya kutokea kwa vifo vya wagombea. Majimbo hayo ni Ulanga Mashariki lililompoteza mgombea kutoka CCM, Celina Kombani; Jimbo la Lushoto lililompoteza mgombea kutoka Chadema, Mohamed Mtoi na Jimbo la Arusha Mjini lililoondokewa na mgombea ubunge kutoka ACT-Wazalendo, Estomiah Mallah.

Aliongeza kuwa uteuzi wa wagombea umeshafanyika katika majimbo ya Ulanga Mashariki na Lushoto na kwamba jana na kwamba, kampeni zitaanza leo hadi Novemba18 huku uchaguzi wao ukitarajiwa kufanyika Novemba 22. Ratiba ya uchaguzi wa Jimbo la Arusha mjini bado haijatolewa.

MNYIKA AISHNGAA NEC
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika, alisema chama chake kiliandika barua wakidai kuwa wapatiwe orodha ya majina ya wapigakura pamoja na idadi ya vituo vya kupigia kura, lakini anashangaa kuona kuwa hilo halikufanyika. 

“Nashangaa barua hiyo nimekabidhiwa leo, lakini haijaeleza ni lini orodha hiyo itapatikana,” alisema.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Tadea, Juma Ali Khatibu, alielezea wasiwasi wao juu ya kutegemea mawasiliano kwa njia ya mkongo wa taifa katika utoaji wa matokeo, akisema kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuchelewesha matokeo na kusababisha usumbufu kwa wapigakura.

Mwenyekiti wa ADC, Said Miraji, alisema kuwa changamoto iliyopo kwa NEC ni kutoaminika kutokana na historia ya viongozi wao waliotangulia, hivyo aliwataka waliopo kuacha tabia ya kulalamika na badala yake watatue matatizo yaliyopo.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Kabendera Eugen, alisema hakuna sababu ya kuwa na hofu na NEC, bali chombo hicho kinapaswa kufuata taratibu na haki.

Akijibu maswali na hoja mbalimbali zilizoibuliwa na viongozi wa vyama, Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhan, alisema kuwa baada ya kutangaza idadi ya wapigakura na vituo, sasa kila kitu kimekamilika na kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwasiliana na NEC ili kupatiwa orodha hizo.

Pia, Kailima aliwatoa hofu viongozi wa vyama vya siasa kwa kuwaleza kuwa mfumo watakaoutumia kutoa matokeo umehakikiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kupitia wataalamu mbalimbali, baadhi wakitoka nchini Ufaransa.

“Kila kitu kitafanyika kwa uwazi. Hivyo hakuna sababu ya kuwa na hofu... kila kitu kitakuwa salama,” alisema
Aidha, alisema uchaguzi ni kazi kubwa na muhimu na kuhusisha wadau wengi, vikiwamo vyama vya siasa, hivyo mafanikio yanategemea ushirikiano mzuri wa NEC na vyama.

Alisema wao wamejipanga kusimamia na kuhakikisha kuwa daima haki inatendeka ili kulinda amani na utulivu na kwamba, kwa sababu hiyo, ni wajibu wa vyama vya siasa kutumia majukwaa yao kuwaelimisha wafuasi wao kutokusanyika jirani na vituo vya kura, bali watekeleze wajibu wao wa kupiga kura na kuondoka.

Mkutano wa jana kati ya NEC na vyama vya siasa ulikuwa na lengo la kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya Uchaguzi Mkuu na pia kupeana taarifa kuhusu maandalizi ya uchaguzi.
CHANZO: NIPASHE

0 Responses to “TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI(NEC) YAFYEKA WAPIGA KURA MILIONI MOJA,WALIOJIANDIKISHA WALIKUWA 23,782,558.”

Post a Comment

More to Read