Thursday, February 4, 2016
WABUNGE WA CCM WAMGOMEA RAIS MAGUFULI
Do you like this story?
Kikao cha siri cha wabunge wa CCM kilichoitishwa juzi usiku
kujadili mipango ya Serikali kudhibiti matumizi, kimefanikiwa kukwamisha uamuzi
wa kuzitaka halmashauri na mashirika ya umma kuingiza mapato yake yote kwenye
mfuko mkuu.
Mpango huo, ambao pia ulipingwa na wabunge kutoka vyama vya
upinzani, ulilenga kuondoa utaratibu uliopo wa halmashauri, mashirika na
taasisi za Serikali kukusanya mapato yake na kuzitumia na badala yake
zilitakiwa ziingize mapato hayo kwenye mfuko mkuu na baadaye Serikali itoe
fedha kulingana na bajeti inazopelekewa.
Juzi, katika mjadala wa mwongozo wa Mpango wa Bajeti ya
Serikali ya Mwaka 2016/17, wabunge hao walipinga uamuzi huo wakisema utaziua
halmashauri na wakataka mashirika ambayo yanamilikiwa na Serikali ndiyo yapeleke
fedha kwenye mfuko huo.
Kutokana na mvutano huo, juzi usiku wabunge wa CCM
walikutana katika kikao cha ndani kilichofanyika makao makuu ya chama hicho
mjini Dodoma, kujadili jambo hilo na kushauri libadilishwe ili kuziokoa
halmashauri nchini.
Jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George
Simbachawene alisema kuwa tayari Serikali imetoa maelezo.
“Tumetoa maelezo kuwa hatukumaanisha halmashauri wala mifuko
ya hifadhi za jamii. Suala hili litayahusu mashirika ya umma pekee,”alisema Simbachawene.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa wabunge
hao walimbana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwamba uamuzi huo
utazifanya halmashauri kukosa fedha za kufanya miradi yake mbalimbali ikwame.
“Mkutano ulianza saa mbili usiku na kumalizika saa tano
usiku. Tulichokubaliana na kufanyika kwa marekebisho ili halmashauri ziendelee
na utaratibu kama wa awali, pia kuitaka Serikali kutoihusisha mifuko ya hifadhi
za jamii katika suala hili,” alisema
mbunge ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
“Fedha zitakazokwenda katika mfuko huo ni za mashirika kama
Tanesco na Tanapa.Lengo hapo ni kuweka utaratibu mzuri wa matumizi kwamba
shirika linaingiza fedha zake katika mfuko, likihitaji fedha litapelekewa
kulingana na utaratibu utakaowekwa.”
Chanzo hicho kilieleza kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii
haitaguswa kwa sababu fedha zake ni za wanachama na hutumika kwa ajili ya
kuendesha miradi mbalimbali.
“Wabunge pia walihoji kama fedha hizo zitaweza kutoka katika
mfuko huo na kuzifikia halmashauri katika kipindi hiki ambacho fedha nyingi
zinashindwa kufika kwa wakati kutekeleza miradi ya maendeleo,”alisema mbunge mwingine.
Jana, katika mjadala wa mpango huo hakuna mbunge wa CCM wala
wa Ukawa aliyegusia suala hilo, kitendo kinachotafsiriwa kuwa jambo hilo
limeondolewa kabisa.
Wachangia mjadala
Akichangia mjadala wa mpango huo, Mbunge wa Lulindi (CCM),
Jerome Bwanausi aliishauri Serikali kuachana na vyanzo vya mapato
vilivyozoeleka, badala yake itafute vyanzo vipya.
Katika mpango huo, Serikali ilitaja baadhi ya vyanzo vyake
vya ndani vya mapato kuwa ni kodi katika vinywaji mbalimbali, sigara, muda wa
matumizi wa simu za mkononi na kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Katika eneo hilo imeweka uwekezako wa kukusanya Sh4
trilioni.“Watendaji wa Serikali lazima wajifunze kutoka katika taasisi
ambazo zina vyanzo vingi vya mapato. Mapato yako mengi tu hata katika nyumba za
kupanga na kuziwezesha halmashauri kukusanya mapato zaidi,” alisema.
Mbunge wa Hanang’(CCM), Dk Mary Nagu alisema uchumi wa viwanda
unategemea kilimo, mifugo na uvuvi na kuitaka Serikali kuhakikisha inatilia
mkazo sekta hizo kwa maelezo kuwa itasaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja
mmoja.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Anatropia Teonist
alionyesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa mipango huo wa Serikali, kutokana na
mawaziri wengi kufanya kazi kwa kutafuta sifa katika vyombo vya habari.
Alimtaja Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi, kwamba anahusika katika uporaji wa viwanja vya wananchi.
“Katika sekta ya ardhi kuna matatizo makubwa. Migogoro ya
ardhi inarudisha nyuma maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa. Pale Dar es Salaam
sasa mnavunja nyumba za watu wa mabondeni. Kutokana na zoezi hilo, zaidi ya
watu 99, 000 watakuwa hawana makazi,” alisema.
Alisema kasi ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo ni
ndogo na kwamba kwa kipindi cha miaka 15, Serikali imepunguza umasikini kwa
asilimia 14 tu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WABUNGE WA CCM WAMGOMEA RAIS MAGUFULI”
Post a Comment