Tuesday, March 15, 2016

POLISI DAR YAKAMATA MAGARI 24 YA WIZI NA DADA & KAKA POA 287




Jeshi la Polisi kanda maalumu ya mkoa wa Dar es Salaam imeendesha oparesheni kali dhidi ya uhalifu mbalimbali na kufanikiwa kukamata watu 287 wenye kujihusisha na masuala ya kuuza miili yao (dada poa na kaka poa), magari 24 ya wizi huku likifanikiwa kukamata mtandao wa watu wenye kujihusisha na wizi wa magari kutoka Dar es Salaam na kuyapeleka mikoa ya kanda ya ziwa

Akizumgumzia mafanikio ya oparesheni hiyo Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya mkoa wa Dar es Salaam, Kamishina simon Sirro alisema jeshi hilo limekuwa likiendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kikazi ambapo safari hii limefanikiwa kuwakamata watu 287 wenye kujihusisha na biashara ya kuuza miili yao jambo ambalo ni kinyume na maadili ya mila za kitanzania.

Kamishna Sirro ameongeza kuwa kuwa licha ya jeshi hilo kuwakamata watu hao kutoka Temeke, Kinondoni na Ilala, jeshi hilo limefanikiwa kuyakamata magari 24 yanayotokana na wizi ambao pia mtandao wake umeweza kubainika na watuhumiwa 50 wamekamatwa.

“Tumefanikiwa kukamata watuhumiwa mbalimbali ambao wanajihusisha na vitendo vya uharifu kwa kuiba magari na kusafirisha kwenda mikoani na uchunguzi zaidi unaendelea ili kuwabaini wote wanaojihusiha,” alisema Kamanda Sirro.

Aidha Kamishna Sirro aliwatoa hofu wakazi wa Dar es Salaam juu ya hali ya usalama kwani jeshi hilo limejipanga vilivyo na kuwataka waendelee kuwa raia wema kwa kutoa taarifa za ualifu kwa vyombo vya usalama ili ziweze kufanyiwa kazi.

0 Responses to “ POLISI DAR YAKAMATA MAGARI 24 YA WIZI NA DADA & KAKA POA 287”

Post a Comment

More to Read