Thursday, August 11, 2016
WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKABIDHIWA MPANGO WA KUHAMIA DODODMA
Do you like this story?
MKOA wa
Dodoma wakishirikiana na Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA)
wametekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kuandaa na kuwasilisha
mapendekezo ya awali ya namna serikali itakavyohamia Dodoma.
Aidha,
imeelezwa kuwa kuanzia sasa Waziri Mkuu ataweka hadharani maelekezo ya wizara
na watumishi kuhamia Dodoma.
Hayo
yamebainishwa katika mahojiano yaliyofanyika jana na Katibu Tawala Mkoa
wa Dodoma, Rehema Madenge.
Mwishoni
mwa mwezi uliopita, Waziri Mkuu wakati akizungumza na viongozi wa serikali,
taasisi, watendaji na wananchi wa Mkoa wa Dodoma alielezea azma ya serikali
kuhamia Dodoma na kutoa siku 14 kwa Mkoa na CDA, kuwasilisha mapendekezo ya
awali kwa namna serikali itakavyohamia Dodoma.
Akitoa
siku hizo kwa Serikali ya Mkoa wa Dodoma kukaa na taasisi zake, hususani CDA
kuandaa na kutoa mpango kazi wake, Majaliwa alisema, “Ndani ya siku 14
nipate proposal (mapendekezo) ya kwanza namna mtakavyotekeleza, naagiza kiundwe
kikosi kazi chini yenu kitakachowajumuisha makundi yote. Baada ya siku 14
nipate mpango wenu.”
Madenge
alisema kwamba Mkuu wa Mkoa huo, Jordan Rugimbana yuko Dar es Salaam
alitarajiwa kuwasilisha mpango kazi huo kwa Waziri Mkuu na kwamba muda wowote
Waziri Mkuu atatangaza utaratibu wa kuhamia Dodoma.
“Tumeandaa
mpango kazi kulingana na maelekezo ya waziri mkuu na mkuu wa mkoa amekwenda
kukabidhi mpango huo,” alisema
Katibu Tawala Dodoma.
Akizungumzia
taarifa za baadhi ya wizara kuanza kuhamia huko, Katibu tawala huyo alisema
kwamba kama mkoa hawana taarifa za wizara na watumishi kuanza kuhamia Dodoma.
“Tunasubiri
maelekezo ya waziri mkuu, baada ya mpango kazi kukamilika utawekwa hadharani
mambo yote ya serikali kuhamia Dodoma,”
alisema Madenge.
Akifafanua
zaidi, alisema anachojua yeye mpango unakabidhiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na na
wizara zitajipanga kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri Mkuu Majaliwa.
Mkoa wa
Dodoma umekuwa katika hekaheka za kutekeleza maagizo ya serikali ya kuhamia
Dodoma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba huduma muhimu kama upatikanaji wa
viwanja zinakwenda kwa taratibu zinazotakiwa.
Ili
kuondoa mhemko na udalali wa viwanja unaoweza kupandisha bei na pia kuzuia
vurugu, mkuu wa mkoa amepiga marufuku uuzaji wa viwanja ndani ya mji wa Dodoma.
Sababu kubwa ya kupiga marufuku kunatokana na kundi la madalali kutoka mikoa
mbalimbali kuvamia mji.
Kupokewa
kwa mpango kazi huo ni moja ya hatua za kukamilisha uhamiaji wa serikali
Dodoma, ambapo hatua nyingine ni kwa serikali kuwasilisha bungeni muswada wa
kuitambua Dodoma kama makao makuu ya nchi ili uthibitishwe kisheria.
Muswada
huo utawasilishwa katika Bunge linaloanza Septemba 6, mwaka huu.
Waziri
Mkuu Majaliwa alisema muswada huo wa sheria ya serikali kuhamia Dodoma,
utapelekwa bungeni ili azma ya Rais John Magufuli na serikali yake uwe na nguvu
kisheria, baada ya Rais Magufuli kutangaza hivi karibuni kuwa ndani ya miaka
minne na ushee iliyobaki ya kumaliza muhula wake wa kwanza wa urais, Serikali
ya Awamu ya Tano itakuwa imehamia katika mji wa Dodoma, ambao mwaka 1973
ulitangazwa kuwa Makao Makuu ya Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)

0 Responses to “ WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKABIDHIWA MPANGO WA KUHAMIA DODODMA ”
Post a Comment