Tuesday, November 1, 2016

WANAFUNZI WAPIGWA RADI WAKATI WAKILA CHAKULA SHULENI MAKETE.





Jumla ya wanafunzi 10 wa shule ya sekondari Mang'oto Kata ya Mang'oto wilayani Makete mkoani Njombe wamejeruhiwa na radi baada ya Mvua iliyoambatana na radi kunyesha shuleni hapo na kuwapiga wanafunzi hao

Akizungumza na Mwandishi wa eddy blog shuleni hapo Mkuu wa shule hiyo Mwl. Bonaventura Mgaya (pichani juu) amesema tukio hilo limetokea Oktoba 30 mwaka huu majira ya saa saba na nusu mchana wakati wanafunzi wakipata chakula cha mchana shuleni hapo

Amesema radi hiyo ilivyopiga wanafunzi wengi walidondoka chini hali iliyowafanya walimu kwenda kuwasaidia na baada ya dakika chache baadhi yao waliweza kuzinduka ndipo walimu walipofanya uchunguzi wa awali kugundua majeruhi na kuwakimbiza kupata huduma za afya katika zahanati ya Mang'oto

Uchunguzi wa wataalamu wa afya katika zahanati hiyo ulibaini mtoto mmoja kujeruhiwa zaidi upande wa kulia wa mwili wake kuanzia begani mpaka mapajani na kulazimika uongozi wa shule kumkimbiza mpaka hospitali ya Consolata Ikonda kwa matibabu zaidi, kabla ya baadaye wanafunzi wengine watatu walioonekana awali kuwa walikuwa na nafuu walizidiwa na kukimbizwa tena katika hospitali hiyo kwa matibabu zaidi

Mwalimu Mgaya pia amezungumzia madhara mengine yaliyotokana na radi hiyo kuwa ni kuunguza mfumo wa umeme wa sola uliokuwa ukitumika shuleni hapo, na mpaka tunakwenda mitamboni shule hiyo haina umeme kwa sasa


Mmoja kati ya wanafunzi waliopigwa na radi hiyo Manfred Mwageni anayesoma kidato cha kwanza shuleni hapo akielezea tukio hilo amesema alishangaa kujikuta ametupwa chini na radi hiyo huku ikiwaunguza wanafunzi wengine

0 Responses to “ WANAFUNZI WAPIGWA RADI WAKATI WAKILA CHAKULA SHULENI MAKETE.”

Post a Comment

More to Read