Thursday, April 27, 2017

Akiri kuua kwa kipigo


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeelezwa kuwa mshtakiwa wa kesi ya mauji, Mwarami Selemani, au Punga, alikiri kumpiga na kumpora Sh. 850,000 na simu ya mkononi, Wiliam Mkumbo (wakati wa uhai wake) ambaye baadaye alikufa kutokana na kipigo hicho.

Kadhalika, mahakama hiyo imeelezwa kuwa mshtakiwa alikiri katika maelezo yake ya onyo alipohojiwa na polisi katika kituo cha Buguruni miaka tisa iliyopita.

Madai hayo yalitolewa jana na shahidi wa nne wa upande wa Jamhuri, Koplo Ernest (52), mbele ya Jaji Lugano Mwandambo anayesikiliza kesi hiyo.


Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali, Anuncitha Leopold na Faraja George.

Akiongozwa na wakili George, shahidi alidai kuwa Januari 21, 2009, akiwa ofisini aliitwa na bosi wake aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wakati huo, Camillius Wambura (kwa sasa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO).

Alidai kuwa alipewa jukumu la kumhoji mshtakiwa wa kwanza, Punga kuhusu tukio la mauaji yaliyotokea eneo la kati ya Sukita na Al Hamza.

Shahidi alidai kuwa alimpa shahidi haki zake zote za msingi ikiwamo kuita ndugu, rafiki au wakili wakati akihojiwa na kutoa maelezo yake ya onyo lakini alikubali kuhojiwa akiwa peke yake.
"Mshtakiwa aliniambia alisoma Shule ya Msingi Buguruni Moto lakini aliishia darasa la tano na kujiingiza kwenye matukio ya wizi wa vyombo vya ndani na nguo.

"Mshtakiwa alinieleza kuwa mwaka 2001, yeye na rafiki zake, aliowataja kwa majina moja moja, Chai Jaba, Salum, Chapapa na Kesi, walibadili mtindo wao na kuanza kupora kwa kutumia silaha ikiwamo nyembe, visu katika kituo cha daladala Chama Buguruni" alidai shahidi.

Aidha, shahidi alidai kuwa mshtakiwa alieleza kuwa waliwavizia watu alfajiri wakati wakienda kazini na waliokuwa wanasafiri na kuwapora vitu mbalimbali vikiwamo pesa, simu za mkononi na nguo.

"Siku ya tukio, mshtakiwa akiwa na Chai Jaba, walidamka alfajiri na kujificha kati ya eneo la Sukita na A Hamza 'tuliona watu watatu mvulana mmoja na wasichana wawili. Yule kijana alituona akaanza kukimbia, tulimzingira tukafanikiwa kumkamata.

Tulimpiga tulimziba matambara ya nguo mdomoni ili asipige kelele alivyotulia tulimsachi tukafanikiwa kupata Sh. 850,000 na simu moja ya mkononi,” alinukuu shahidi maelezo ya mshtakiwa.

Akifafanua zaidi alidai kuwa mshtakiwa alidai kuwa walimwacha kijana yule akiwa kwenye hali mbaya na kutoweka eneo la tukio na kwamba waligawana fedha na simu alikwenda kuuza Ilala kwa Chogo.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, baada ya tukio hilo, mshtakiwa alijificha maeneo ya Kitunda nyumbani kwa wazazi wake na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi.

Upande wa Jamhuri ulifunga ushahidi wao baada ya kuita mashahidi wanne na vielelezo vitatu ikiwamo ripoti ya daktari na maelezo ya washtakiwa kukiri kuhusika na mauaji hayo.

Mbali na Punga, mshtakiwa mwingine ni, Rashidi Mbepu maarufu kama China.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Novemba 7, 2008, eneo la Tabata Matumbi, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walimuua William Mkumbo.

0 Responses to “Akiri kuua kwa kipigo ”

Post a Comment

More to Read