Thursday, April 27, 2017

Nay wa Mitego apigwa onyo kali na Ustawi wa Jamii


Kutokana na wanawake kadha wa kadha kujitokeza na kudai kwamba wamezaa na staa wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ lakini amewatelekeza, Idara ya Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam, imemuonya jamaa huyo na kumtaka kuwa makini katika hilo.
Ustawi wa jamii wamesema suala la Nay kutelekeza watoto linaweza kumletea matatizo kama vile kifungo jela au kulazimishwa kumlea mtoto husika hadi akue na kuweza kujitegemea.
“Anachokifanya Nay siyo kitu kizuri kabisa kwani kwanza anawadhalilisha wanawake kwa kuzaa nao, halafu hawahudumii.
“Suala la kutelekeza watoto linaweza kumsababishia kifungo au kutoa matumizi kwa lazima kama wahusika, yaani wanawake waliozaa naye watachukua hatua za kisheria hivyo anatakiwa abadilike sana,” alisema afisa huyo aliyetambulika kwa jina moja la Janeth.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kulikuwa na kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ‘birthday’ ya mtoto wa Nay aliyezaa na mwigizaji wa sinema za Kibongo, Skyner Ally ‘Skaina’ ambapo mwanamuziki huyo alimtakia heri katika kukua kwake huku akiweka picha na maneno kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Hali ilichafuka baada ya Skaina kuandika waraka mrefu kwenye ukurasa wake wa Instagram akiambatanisha na picha akiwa na mwanaye na kumtaka Nay kuacha kumshobokea mwanaye kwani ni miaka mitano sasa hajui anavaa nini, anakula nini wala anaishi vipi yeye amekalia kuposti picha za mtoto huyo tu wakati ni baba kwa jina tu.
“Baba jina anakufanyia promosheni kudanganya Watanzania kama ohoo my twin, sijui nanunua pisto, hata nguo ya ndani unayovaa hajui thamani yake, nimevumilia sana miaka mitano sasa nimejisikia kutapika na Mungu nakuomba unijalie maisha marefu, uwezo, nizidishie riziki, uzima na afya nikulee mwanangu aje akuone baadaye umekuwa waziri halafu alete pua yake sijui itakuwaje.
“Mungu akuweke uje uone mafanikio ya mwanangu, endelea na drama zako ila tafadhali shobo na mwanangu sitaki, unaposti picha za mtoto wangu za nini, sitaki shobo na mwanangu, je, wababa wanaojisifu kama wanawapenda watoto wao halafu hata hawajui mtoto anakula nini, anasoma wapi, anavaa nini, wapooo….
“Nilikuwa na dukuduku moyoni ndani ya miaka mitano nimeongea na limetoka ukweli, unamuweka mtu huru, kutwa kucha kuwadhalilisha wenzio ya kwako yanakushinda, usiwafunze wenzio, jifunze kwanza kwako,” aliandika Skaina.
Baada ya waraka huo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Nay ili kumsikia anazungumziaje hilo ambapo alisema hawezi kuzungumza juu ya suala hilo.
“Siwezi kuzungumzia chochote kuhusiana na hilo,” alisema Nay.
Mbali na Skaina, wiki kadhaa zilizopita msanii wa Bongo Fleva, Faidha Omary ‘Sister Fay’ naye aliibuka na kudai kuzaa na Nay huku akisema kwamba amemtelekeza, lakini alipoulizwa Nay mwenyewe alikataa katakata kwamba mtoto huyo siyo wake.

0 Responses to “Nay wa Mitego apigwa onyo kali na Ustawi wa Jamii ”

Post a Comment

More to Read