Friday, June 27, 2014
UKEKETAJI WATAJWA KUWA MWIBA MCHUNGU KWA WANAWAKE NCHINI
Do you like this story?
SERIKALI
imesema kitendo cha baadhi ya makabila kuendeleza mila za kuwakeketa wanawake
na watoto ni ukatili mkubwa ambao umekuwa na madhara kiafya kwa anayetendewa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maendeleo ya Jamii
Jinsia na Watoto, Sophia Simba alipokuwa akifungua Mkutano wa Kitaifa wa
Kujadili Utokomezaji wa Ukeketaji nchini Tanzania unaofanyika kwa siku mbili
katika Mkumbi wa Mikutano wa Kunduchi Hoteli.
Waziri Simba
alisema ukeketaji ni udhalilishaji wa wanawake na watoto wa kike na umekuwa
ukihatarisha maisha ya wahusika kwa matokeo ya vifo, vilema na maradhi kama
vile fistula na magonjwa mengine hivyo kutaka kila mmoja kuungana kuupinga.
Alisema kwa upande wa Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali ili
kuhakikisha inatokomeza mila hizo pamoja na ukatili mwingine wa kijinsia.
“Wengi hapa
ni mashaidi wa madhara ya ukeketeji ikiwemo vifo, vilema na maradhi kama vile,
fistula na mengineyo. Serikali inalaani na kukemea ukatili huu unaomdhalilisha
mwanamke na kumletea madhara makubwa,” alisema Waziri Simba. Aidha alisema ili
kupambana na hali Serikali imesaini mikataba mbalimbali ya kukabiliana na
ubaguzi anuai hasa kwa wanawake na pia kuanzisha Dawati la Jinsia kila sekta
kukabiliana na vitendo vya kikatili nchini. “…Serikali iliandaa na inatekeleza
mpango wa taifa wa kuzuia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto
(2001-2015) na mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukeketaji (2001-2015)…,”
alisisitiza Waziri Simba.
Aliongeza
pamoja na hayo na juhudi mbalimbali za Serikali ukatili huo kwa wanawake na
watoto hauwezi kuzuiliwa kwa sheria na mipango ya serikali hivyo kuitaka jamii
pamoja na wadau wengine kuunganisha nguvu kupambana na vitendo hivyo hapa
nchini. “….Suala la kutokomeza ukatili wa kijinsia, halitakwisha kwa kutegemea
Serikali au sheria peke yake. Ni jukumu letu wadau wote kwa pamoja kukemea na
kupiga vita kwa nguvu zote, kutoa elimu dhidi ya ukatili, huduma kwa wahanga na
kuhakikisha wanaotenda na kubariki vitendo hivi wanachukuliwa hatua,” alisema.
Akizungumza
katika mkutano huo, Naibu Mwakilishi wa UNFPA Tanzania, Mariam Khan alisema
licha ya juhudi zinazofanywa kupambana na ukeketaji nchini, kila mwaka vipindi
vya ukeketaji bado wasichana na watoto wanaokeketwa wamekuwa wakipoteza maisha
bila sababu ya msingi kutokana na madhara ya ukeketaji jambo ambalo haliwezi
kuvumiliwa. Aliwataka washiriki kwa pamoja kujadiliana nini cha kufanya ili
kukomesha ukatili huo unaoendelea kushamiri nchini na kuahidi kuwa UNFPA
itaendelea kuunga mkono juhudi za mapambano hayo kwa kutoa mafunzo na kuwezesha
shughuli za mapambano hayo.
Awali
akizungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania
(TAMWA), Valerie Nsoka alisema mkutano huo umewashirikisha wakuu wa mikoa,
viongozi wa dini, wawakilishi wa madawati ya jinsia na wadau wengine kutoka
mikoa yenye vitendo vya ukeketaji pamoja na asasi zinazopambana na ukeketaji.
Aliongeza kuwa mkutano huo utafanyika kwa siku mbili ambapo wajumbe, watapeana
uzoefu na kufanya majadiliano ya kina kabla ya kuibuka na mpango kazi wa nini
kifanyike kutokomeza vitendo vya ukeketaji nchini. Mkutano huo ulioratibiwa na
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) umefadhiliwa na Shirika la
UNFPA, Tanzania. *Imeandaliwa na www.thehabari.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ UKEKETAJI WATAJWA KUWA MWIBA MCHUNGU KWA WANAWAKE NCHINI ”
Post a Comment