Thursday, August 21, 2014
MGOMO MPYA WA WAFANYABIASHARA WA JIJI LA MWANZA WAANZA RASMI LEO:MKURUGENZI ADAIWA KUWAKIMBIA,TRA WATISHIA KUWAFUNGIA LESENI ZAO
Do you like this story?
Wafanyabisahara
jijini Mwanza leo wameanza mgomo wa kutofungua maduka yao kwa siku
zisizojulikana kwa kile walichodai Mkurugenzi wa jiji hilo, Hassan Hida
amekataa kukutana nao kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili.
Mgomo huo
utakuwa wa pili kufanyika baada ya mara ya kwanza kutokea wakati
wafanyabiashara hao wakigomea matumizi ya mashine za Stakabadhi za
Elekitroniki (EFD).
Hata hivyo
mgomo huu ulioanza leo hauhusishi tena mashine za EFD badala
yake umejikita katika matatizo yanayowakabili ambayo ni ongezeko la kodi
ya taka kutoka Sh 8,000 hadi 10,000, kutoza fedha za kuweka bidhaa zao nje ya
duka na mambo mengine ya kukamatiwa mali zao.
Uamuzi huo
ulifikiwa juzi katika mkutano mkuu ulioitishwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara
Tanzania (JWT), mkoa wa Mwanza kwa lengo la kutoa taarifa za mazungumzo kati ya
Serikali juu ya matumizi ya mashine za EFD.
Kabla ya
kufikia azimio la kutofungua maduka yao, Mwenyekiti wa JWT, mkoa wa Mwanza,
Christopher Wambura aliwaeleza wafanyabiashara hao jitihada alizofanya za
kukutana na mkurugenzi huyo mara zote ziligonga mwamba.
“Ndugu
zangu wafanyabiashara mliniagiza pamoja na viongozi wenzangu tutafute suluhisho
la matatizo yanayotukabili katika biashara zetu hapa jijini Mwanza, wakati
tunahangaika hapa kwetu, viongozi wa kitaifa wa JWT nao walikuwa wanahangaika
huko Dar es Salaam.
“Kwa
bahati nzuri uongozi wa kitaifa umefanikiwa kwenda Ikulu na kukutana na
wawakilishi wa Rais Jakaya Kikwete, baada ya hapo walikutana na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda pamoja na viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ndio
maana leo mnaona hakuna usumbufu juu ya mashine za EFD.
“Wakati
usumbufu wa EFD ukiwa umepotea, kero zetu zinazotukabili hapa Mwanza bado
hazitaki kutatuliwa na uongozi wa jiji, mkurugenzi anatukimbia kila tunapopanga
kukutana naye.
“Tumefanya
jitihada za kukutana na Mkuu wa Mkoa, Evarist Ndikilo, Mkuu wa Wilaya ya
Nyamagana, Baraka Koni na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Titto Mahinya wote
walionyesha jitihada za kutusaidia kukutana na mkurugenzi lakini hatukukutana
mpaka leo hii,”alisema.
Wambura alisema
pamoja na jitihada hizo, mara zote mkurugenzi amekuwa akiwaeleza kutokuwa na
nafasi ya kukutana nao kwa kile alichodai kubanwa na majukumu ya kazi pamoja na
kuwa nje ya mkoa kwa shughuli maalumu.
Pamoja na
masuala mengi yaliyozungumzwa hapo, wafanyabiashara na viongozi wao
walikubaliana kutofungua maduka yao hadi hapo mkurugenzi atakapokutana nao huku
wakisisitiza na kutoa onyo kwa wale watakaokiuka maazimio yao.
Mkurugenzi
anena
Mpekuzi
ilimtafuta Mkurugenzi wa jiji hilo kwa njia ya simu, ambapo alisema yupo nje ya
ofisi, lakini amewataka viongozi wa JWT
wakutane naye kesho saa nne ofisini kwake.
“Nipo
nje ya ofisi, muda huu siwezi kuzungumzia mgomo huo, lakini
nimewaomba wafungue maduka yao halafu Viongozi
wao wafike Ofisini kwangu kesho saa
nne tuzungumze,”alisema kwa
ufupi.
TRA
Mwanza
Kwa upande wa
Meneja wa TRA mkoa wa Mwanza, Jeremia Lusana amesema kitendo cha
wafanyabiashara hao kugoma kinasababisha hasara kubwa katika suala la mapato
huku akitishia kuwafungia lenseni za biashara zao.
“Tumechoka
kutishwa na mgomo wa wafanyabiashara hao, umefika muda wa kuangalia namna ya
kuwafungia leseni zao ili wakae nyumbani, biashara yao ina manufaa kwao na
sisi, kipindi kile tulipata hasara kwa sababu mgomo ulishtukiza."Amesema Lusana
Lusana
amesema TRA haina uwezo wa kuwalazimisha kufungua maduka, hivyo
watasubiri hadi hapo watakapofungua ndipo watakapoendelea na shughuli zao
ukusanyaji mapato kwao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MGOMO MPYA WA WAFANYABIASHARA WA JIJI LA MWANZA WAANZA RASMI LEO:MKURUGENZI ADAIWA KUWAKIMBIA,TRA WATISHIA KUWAFUNGIA LESENI ZAO”
Post a Comment