Wednesday, August 6, 2014
MKE, MUME WAKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA.
Do you like this story?
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limewakamata
watu watano wakiwa na magunia saba ya madawa ya kulevya aina ya bhangi
wakiwemo mke na mume. Awali askari wa Kitengo cha Kuzuia Madawa ya Kulevya
Mkoani hapa wakiwa doria walipata taarifa toka kwa raia wema iliyoeleza kuwepo
kwa watu wanaosafirisha madawa hayo.
Mara baada ya kupata taarifa hiyo askari hao
waliweka mtego maeneo ya Sanawari ambapo muda wa saa 3:30 usiku walifanikiwa
kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Hussein Rashid (35) mkazi wa Sakina,
dereva pamoja na mwenzake Sebastian Wilbert (37) Fundi magari, mkazi wa Ilboru
wakiwa wanasafirisha magunia matano ya madawa ya kulevya aina ya bhangi yenye
uzito wa kilogramu 171 kuelekea nchi jirani ya Kenya kwa kutumia gari aina ya
Toyota Corolla lenye namba za usajili T. 589 AZS.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus
Sabas alisema kwamba, mara baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa walikiri kosa hilo
na kumtaja mwanamke aitwaye Flora John (38) Mkazi wa Ekenywa- Ngaramtoni kuwa
ndio aliyewauzia.
Kamanda Sabas aliendelea kwa kusema kwamba, askari
hao walianza kumfutilia mwanamke huyo ambapo jana Jumanne tarehe 05.08.2014
walikwenda nyumbani kwake na kumkuta mtuhumiwa ambaye ni muuzaji akiwa na
mume wake aitwaye John Meleji (45) Mkazi wa Ekenywa na mara baada ya kufanya
upekuzi walikuta gunia moja la madawa ya kulevya aina bhangi ndani ya nyumba
hiyo.
Mbali na kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni mke na
mume pia askari hao walimkamata jirani yao aitwaye Loseriani Metelami (21)
Mkulima mkazi wa Ekenywa baada ya yeye pia kukutwa na gunia moja la madawa ya
kulevya aina ya bhangi hivyo kufanya jumla ya magunia yaliyokamatwa kuwa saba.
Watuhumiwa hao watano wanatarajiwa kufikishwa
mahakamani hivi karibuni mara baada ya upelelezi kukamilika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MKE, MUME WAKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA.”
Post a Comment