Thursday, August 7, 2014

WARIOBA:BUNGE LITAPOTEZA FEDHA ZA WANANCHI ENDAPO HAKUNA MARIDHIANO.




Dar es Salaam. Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema kuendelea vikao vya Bunge Maalumu la Katiba bila kuwapo maridhiano baina ya pande zinazovutana na upande mmoja ukibaki nje ya Bunge, ni sawa na kutumia vibaya fedha za Watanzania.

Amesema kauli kwamba akidi ya wajumbe wa Bunge hilo imetimia na vikao vinaweza kuendelea haiwezi kuzaa Katiba itakayokubaliwa na wananchi wote na ni tofauti na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inavyoeleza katika sehemu ya kufanya uamuzi.

Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wetu ofisini kwake Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema, “Kama uwezekano wa kukutana upo, kwa nini Bunge liendelee kutumia fedha wakati mnajua kuwa mwisho hamtafikia uamuzi? Jambo la msingi ni kujitahidi kuafikiana na Bunge liwe na wajumbe wote.”

Kauli ya Warioba imeungwa mkono na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba wakati akichangia hoja ya mabadiliko ya kanuni ya Bunge hilo kwa kulitaka bunge hilo kujitathimini iwapo baada ya mjadala litaweza kufikia uamuzi, ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha za walipakodi.

Akitoa hadhari hiyo bungeni jana, Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, alisema ni vyema Bunge hilo likajiridhisha kuhusu namna linavyoweza kutumia siku 60 zilizowekwa kwa uhakika na umuhimu wa kuziondoa siku za Jumamosi kitendo kinachosababisha kuongezeka hadi kufikia 84.

“Tujiridhishe na kukubali ukweli kwamba kukaa hapa kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili inayohitajika kupitisha rasimu hii haiwezi kueleweka kwa Watanzania. Ni lazima Watanzania watatuuliza tumefanya nini,” alisema.

Alisema kwa namna moja, ni vyema kujua idadi halisi ya wale wanaoshiriki katika awamu ya pili ya Bunge hilo na wale wasioshiriki, ili kutoa uthibitisho wa kihesabu kwamba uamuzi wa kuendelea kwa bunge unaweza kuwa na maana.

Hata hivyo, Nchemba alisema ni vyema wakiendelea kujadili masuala muhimu na kwa kuwa wanakwenda kujadili sura muhimu zinazogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania, lakini kwa uhakika kwamba hatua hiyo itakuwa na manufaa kwa Watanzania katika hatua ya mwisho.

Alisisitiza kwamba iwapo hatua hiyo itashindikana, utetezi wa mwisho hautaweza kueleweka kwa sababu suala la kutimia kwa akidi kwa mujibu wa Katiba ni muhimu katika kufikia uamuzi na hasa kuangalia upya umuhimu wa kufikia maridhiano kwa sasa.
Bunge la Katiba lilianza jana mjini Dodoma bila kuwapo kwa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na baadhi ya wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais waliosusa vikao hivyo.

Ukawa wanashinikiza kujadiliwa kwa rasimu ya Katiba iliyotolewa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na si ile iliyodai inaingizwa kinyemela na wajumbe wanaounga msimamo wa CCM wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa na rasimu.
Licha ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kuitisha kikao cha mashauriano kati yake, CCM na Ukawa, mwafaka haukupatikana.
Via>Mwananchi

0 Responses to “WARIOBA:BUNGE LITAPOTEZA FEDHA ZA WANANCHI ENDAPO HAKUNA MARIDHIANO.”

Post a Comment

More to Read