Tuesday, September 30, 2014

WATU 270 WALAZWA KWA KUNYWA TOGWA.



Pombe aina ya Togwa


Watu  watano wakazi wa kijiji cha Litapwasi wilaya ya Songea wanashikiliwa na polisi Mkoani Ruvuma kwa mahojiano zaidi kufuatia watu 246 kulazwa katika hospitali ya Misheni Peramiho na kituo maalumu kilichoandaliwa katika zahanati ya kijiji cha Ligweneni baada ya kunywa togwa ya kienyeji inayodhaniwa kuwa na sumu.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Ruvuma Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo limetokea jana mchana katika kijiji cha Litapwasi  nyumbani kwa Ines Nungu (47) ambako kulikuwa na sherehe ya ubarikio wa kipaimara cha watoto wake 2.

Kamanda Msikhela amesema kuwa katika sherehe hiyo kulikuwa kumeandaliwa vyakula mbalimbali, vinywaji ikiwemo togwa iliyotengenezwa kienyeji ambayo imeonekana kuwa watu wengi ambao waliohudhuria kwenye sherehe hivyo walikunywa kwa wingi.

Alisema katika sherehe hiyo ambayo ilihudhuriwa na watu wengi kutoka sehemu mbalimbali za vijiji vya Liagweni,Sinai,Likulufusi na Songea Mjini kulikuwa na kinywaji cha togwa ambacho walikuwa wakijihudumia wao wenyewe pale wanapohitaji.

Alifafanua kuwa katika sherehe hiyo kulikuwa na vyakula vingi pamoja na togwa lakini inaonekana kuwa watu waliokula vyakula bila ya kunywa togwa hawakuathirika na hali zao zinaendelea vizuri.

Alisema baada ya muda mfupi watu waliokunywa na kutawanyika kurudi majumbani kwao ambako walianza kuharisha na kutapika.

Baada ya kuwepo  taarifa ya tukio hilo baadhi ya waathirika walikimbizwa katika hospitali ya Misheni ya Peramiho wengine walikimbizwa katika zahanati ya kijiji cha Liagweni na baadhi ya waathirika ambao idadi yake haifahamika walikimbilia kwa waganga wa kienyeji.

Alieleza kuwa walioripotiwa kupokelewa katika Hospitali ya misheni ya Peramiho mpaka  mchana walikuwa 77 lakini watu 27 wamelazwa na hali zao bado ni mbaya na wengine walitibiwa na kurudi majumbani mwao.

Alifafanua zaidi kuwa waathirika wengine 169 wamepokelewa na kulazwa katika kituo maalum kilichoandaliwa kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ugonjwa wa kuharisha na kutapika kilichopo katika zahanati ya Liagweni kati yao watu 10 hali zao ni mbaya ambapo jumla ya wagonjwa 246 ndiyo idadi ya waathirika waliopelekwa kwenye hospitali ya Misheni ya Peramiho na kwenye kituo maalum kilichopo katika zahanati ya Liagweni.

Kamanda Msikhela amesema kuwa kufuatia tukio hilo watu 5 wanashikiliwa na polisi akiwemo mwandaaji wa sherehe hiyo Ines Nungu na chanzo cha sababu ya togwa hiyo kuwekwa sumu kinafanyiwa uchunguzi zaidi.

Na Gideon Mwakanosya, jamvi la habari Songea

0 Responses to “WATU 270 WALAZWA KWA KUNYWA TOGWA.”

Post a Comment

More to Read