Tuesday, September 30, 2014

MEYA AGIZA POLISI KATA KUWAKAMATA WANAOCHIMBA MCHANGA PEMBEZONI YA BARABARA MKOLANI




MEYA wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkolani (CCM), ameagiza Polisi katani humo kuwakamata wanaochimba mchanga kondo ya barabara ya Nyahingi na Nyamazobe mlimani na kusababisha uharibifu mkubwa.

Akizungumza juzi kwenye mkutano wa hadhara eneo la Mkolani, Mabula,  alisema uharibifu huo umesababisha barabara hizo kutopitika kirahisi na kuhatarisha  watumiaji na magari na hata mitambo ya Jiji ambayo imekuwa ikishindwa kutengeneza barabara hizo kwa kuhofia kuporomoka na kuharibika kutokana na mashimo makubwa.

“Naombeni wananchi tushirikiane kwa hili kwani kumekuwa na kero kubwa ya barabara kwa wananchi wa mitaa hiyo kutokana na shughuli za uharibifu zinazofanywa za ufyatuaji matofari na uchimbaji wa mchanga pembezoni mwa barabara hizo jambo ambalo ni lazima lisitishwe haraka ili Halmashauri itekeleze jukumu la kutengeneza barabara hizo,”alisema.

Mabula alisema Halmashauri ya Jiji inayo mitambo miwili tu ambayo ni Kijiko na Katapila ambavyo kwa sasa havitoshelezi kwa sasa katika mahitaji muhimu ya kuzifanyia ukarabati na matengenezo barabara za mitaa katika Kata 12 za Jimbo la Nyamagana.

“Tumekuwa tukitoa mitambo hiyo kwa zamu ambapo  kila Kata huitumia kwa siku tatu, ambayo bado haitoshelezi na hali ya barabara zetu za mitaa ziko kwenye hali mbaya hivyo ni vyema mitambo hiyo inapokuja kutengeneza barabara hizo wananchi mtoe ushirikiano ili kufanikisha na kusaidia barabara kupitika kirahisi,” alisisitiza.

Meya Mabula , akijibu hoja za baadhi ya wananchi alisema mgogoro wa ardhi eneo la Block E ambalo kuna mmiliki ameshindwa kuliendeleza eneo hilo kisheria ambalo ni eneo la uwekezaji wa viwanda na tumewasilisha ombi la kutenguliwa umiliki wa eneo hilo kwa sasa ili tuweze kuligawa kwa wananchi na kuliendeleza na kupitisha barabara ili wananchi wa jirani wapate huduma.

“Nawaahidi kupambana ili kuhakikisha kunapatikana barabara za kufika katika maeneo ya jirani ambayo niya wananchi kutokana na mmiliki huyo kushindwa kutekeleza hilo kwa muda mrefu na Jiji lilishindwa kutengeneza barabara kutokana na mmiliki huyo kuzuia na hivyo njia pekee ni kurejea kwenye sheria na kumomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kufuta hati ya umiliki huo.

Mabula pia aliwahakikishia wananchi wa eneo la Nyamazobe milimani kutekeleza hahadi yake ya kuwafikishia maji safi ambapo mchakato wake unashughulikiwa kwa pamoja na wataalamu wa Jiji na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka na Mazingira (MWAUWASA) na kuhusu Hati za maeneo ya wananchi wa eneo hilo tayari ramani ya maeneo 102 imepitishwa na sasa wananchi watapewa utaratibu wa kupata Hati zao.

0 Responses to “MEYA AGIZA POLISI KATA KUWAKAMATA WANAOCHIMBA MCHANGA PEMBEZONI YA BARABARA MKOLANI”

Post a Comment

More to Read