Thursday, November 6, 2014
RAIS KIKWETE AFANYA UTEUZI WA WAKUU WA MIKOA.
Do you like this story?
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu wapya wanne
wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine watatu watapangiwa
kazi nyingine.
Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma jioni
ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
inasema kuwa, Wakuu wapya wa Mikoa ni Bi. Halima Omari Dendego ambaye anakuwa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim Hamisi Msengi
ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza ambaye anakuwa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu wa
Mkoa wa Kagera.
Taarifa inasema kuwa kabla ya uteuzi
wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dkt. Msengi alikuwa Mkuu wa
Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Bwana
Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo inasema kuwa Wakuu hao
wapya wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6, 2014 saa saba mchana,
Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu
wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali (Mst) Fabian Massawe wa
Kagera, Dkt. Christine Ishengoma wa Iringa na Kanali Joseph Simbakalia wa
Mtwara.
Wakuu wa Mikoa ambao wamehamishwa
vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda Mkoa wa Mwanza
kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa wa Njombe kutoka
Dodoma, Bwana Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kepteni
(Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na Mhandisi Everist
Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.
Wengine waliohamishwa ni Luteni (Mst)
Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dkt.
Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka Katavi, Bi Fatma Mwasa
ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka Tabora na Bwana Magalula S.
Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita.
Taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa
Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya,Morogoro, Pwani,
Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya
sasa.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa
Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi.
Taarifa kamili itatolewa na Waziri
Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya mink moo Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
05 Novemba,2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS KIKWETE AFANYA UTEUZI WA WAKUU WA MIKOA.”
Post a Comment