Thursday, January 28, 2016
WATUHUMIWA 7 WA MAKONTENA WALIOTOROKA WAKAMATWA
Do you like this story?
Wafanyakazi
saba kati ya wanane wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) waliotuhumiwa
kuhusika kutorosha makontena 11,019 na magari 2,019 kutoka bandarini ambao
walitoroka, wamepatikana na tayari wanaendelea kuhojiwa na polisi juu ya tuhuma
hizo.
Watumishi hao
ni kati ya watuhumiwa 15 wa TPA waliotangazwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuwa wameshiriki kuondosha makontena na
magari hayo kutoka katika bandari kavu saba bila kulipa ushuru wa Bandari.
Meneja Mawasiliano
wa TPA, Janet Ruzangi alisema jana kuwa mfanyakazi mmoja kati ya hao wanane,
hajapatikana; na anaendelea kusakwa na polisi ili afikishwe kwenye vyombo vya
sheria.
“Wote
walishapatikana kasoro mtumishi mmoja, Happygod Naftali, ambaye huyu alishaacha
kazi siku nyingi baada ya viongozi kuanza kufuatilia suala hilo; lakini bado
polisi wanaendelea kumsaka,”
alisema Ruzangi.
Mkuu wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alithibitisha watuhumiwa hao,
kukamatwa na kwamba bado wanaendelea kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo.
“Ni
kwamba tunaendelea na upelelezi wetu,”
alisema Sirro licha ya kuwa hakutaka kutaja idadi ya wafanyakazi wa TPA ambao
wamepatikana.“Kwa kweli idadi nitaitoa siku nitakapozungumza na waandishi wa
habari wiki hii,” alifafanua.
Watumishi
waliokuwa wanasakwa na polisi waliopatikana kwa mujibu wa Ruzangi ni Aron
Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Bonasweet Kimaina,
Zainab Bwijo na Nathan Edward.
Watumishi hao
wanaungana na watumishi wengine saba John Elisante, Leticia Masaro, Christina
Temu, Merina Chawala, Adnan Ally, Masoud Seleman na Benadeta Sangawe
waliokamatwa na kuhojiwa kuhusu sakata hilo. Watumishi hao saba, kwa mujibu wa
Sirro, tayari walishapelekwa mahakamani.
“Ukiacha
wale saba ambao tumeshawafikisha mahakamani, hawa wengine bado tuko nao
tunaendelea kufanya upelelezi,”
alieleza.
Wafanyakazi hao
wanatuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,884 na magari 2,019 ambayo
yalitoroshwa kutoka katika Bandari Kavu (ICD) saba bila kulipiwa ushuru wa
bandari na hivyo kuipotezea Serikali mapato ya Sh bilioni 48.55.
Kuhusu mawakala
280 waliopewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo yao makao makuu ya TPA namna
ya walivyohusika kulipia makontena hayo, Ruzangi alisema mamlaka yake
inajipanga kutoa taarifa kamili juu ya suala hilo.
“Tunaendelea
kuandaa taarifa ya kilichotokea na kilichobainika kuhusu mawakala hao, tutatoa
taarifa hivi karibuni,” alisema Meneja
Mawasiliano huyo.
Tangu Rais John
Magufuli aingie madarakani, uongozi wake umeibua ufisadi wa kutisha ambao
ulikuwa unafanywa Bandari ya Dar es Salaama kwa kuwashirikisha wafanyakazi wa
TPA na mawakala pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Kwa mara ya
kwanza upotevu wa makontena 349 uligundulika baada ya Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa kutinga bandarini na kubaini makontena hayo kutolewa bandari kavu bila
kulipiwa kodi.
Upotevu huo
ulifanya vigogo wa TRA, akiwemo Kamishna Mkuu Rished Bade na makamishna wengine
kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani.
Baadaye
Majaliwa alibaini upotevu wa makontena 2,431 yaliyoondolewa bandari kavu bila
kulipiwa ushuru wa Bandari.
Katika sakata
hilo, baadhi ya mawakala wa forodha walifungiwa kufanya biashara na TPA Sakata
la mwisho ni la kupotea kwa makontena 11,019 na magari 2,019, ambayo
yaliondolewa kwenye ICD saba bila kulipiwa ushuru wa bandari na kuipotezea
serikali mapato ya Sh bilioni 48.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WATUHUMIWA 7 WA MAKONTENA WALIOTOROKA WAKAMATWA”
Post a Comment