Wednesday, July 27, 2016

WAUMINI NA MAASKOFU KUFANYA USAFI JIJINI MBEYA


Mwenyekiti wa kamati ya Ushauri wa Makanisa ya Pentekosti Mkoa wa Mbeya, Askofu Dk. Donald Mwanjoka, akizungumza na watendaji wa kata zote za jiji la Mbeya.

Watendaji wa Mitaa wakisikiliza kwa Makini.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Bw William Ntinika Paul akitoa  Neno Mbele ya watendaji na Viongozi wa Dini.


Meya wa Jiji la Mbeya Mch David Mwashilindi akitoa Shukrani kwa Uongozi wa Dini kwa kujitolea Kufanya Usafi jijini Mbeya siku ya Ijumaa.(Picha na Dvid Nyembe wa Fahari News)



VIONGOZI na Waumini wa madhehebu ya Kikristo mkoani Mbeya wanatarajia kufanya usafi kuzunguka viunga mbali mbali vya Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli la kuhamasisha usafi wa mazingira.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika  katika ukumbi wa Hoteli ya Paradise Soweto jijini Mbeya, Mwenyekiti wa kamati ya Ushauri wa Makanisa ya Pentekosti Mkoa wa Mbeya, Askofu Dk. Donald Mwanjoka alisema usafi huo utafanyika Julai 29, mwaka huu kuanzia majira ya asubuhi.

Dk. Mwanjoka alisema lengo la kufanya usafi ni kuhamasisha jamii na kuunga mkono jitihada za Serikali za kufanya usafi sambamba na maandalizi ya kuelekea kwenye mkutano mkubwa wa Injili unaotarajiwa kufanyika kwa siku tatu katika viwanja vya Shule ya Msingi RuandaNzovwe kuanzia Agosti 4 hadi 7,2016.

Alisema katika zoezi hilo la usafi wananchi wote wameshirikishwa kupitia viongozi wa Serikali za Mitaa na Kata ambapo kikao cha maandalizi kimeshafanyika kikiwashirikisha Meya, Mkurugenzi wa Jiji na viongozi wengine.

Naye Askofu John Mwela ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakristu Mkoa wa Mbeya alisema kupitia mkutano mkubwa wa injili utakaomleta mhubiri wa kimataifa, Daniel Kolenda ambao awali ulilenga madhehebu ya Kipetekosti lakini sasa wameamua kushirikisha madhehebu yote ili ujumbe uwafikie wananchi wote.

Alisema kupitia mkutano huo ambao unafanyika Mbeya kwa mara ya pili  tangu mwaka 1992 Wakazi wa Mbeya watabadilika kutokana na kuhubiriwa amani na kuhamasishwa kufanya kazi kwa bidii ili kuondokana na vitendo viovu.

Aliongeza kuwa mhubiri huyo wa kimataifa anakuja mkoani Mbeya kusaidia kuhamasisha wananchi na watanzania kuachana na vitendo viovu na kuimarisha amani ambayo haipatikani kwa mtutu wa bunduki bali kwa mahubiri.

Akizungumzia kukithiri kwa vitendo viovu nchini hususani Mkoa wa Mbeya alisema viongozi wa dini ndiyo wenye jukumu la kuhubiri amani hivyo kuongezeka ama kupungua kwa maovu kunasababishwa na viongozi wa dini kushindwa kukemea uovu waziwazi.

Alisema pia kupitia mkutano huo huduma mbali mbali za kijamii zitafanyika ikiwa ni pamoja na kutembelea watoto wasiojiweza, magarezani na kutoa msaada wa mahitaji mbali mbali pamoja na maombezi maalum.

0 Responses to “WAUMINI NA MAASKOFU KUFANYA USAFI JIJINI MBEYA”

Post a Comment

More to Read