Wednesday, July 27, 2016
WAZIRI MHAGAMA NA MANAIBU WAKE KUHAMIA DODOMA WIKI IJAYO
Do you like this story?
Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Uratibu,Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu itahamia
Dodoma juma lijalo kufuatia agizo la Mhe. Rais John Pombe Magufuli la Serikali
kuhamia Dodoma.
Kauli hiyo
imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Uratibu, Bunge, Kazi ,Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista
Mhagama wakati akiongea na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi
zilizoko chini ya ofisi hiyo.
“Mchakato
wa kuhamia Dodoma umekwisha kilichobaki kwa sasa ni utekelezaji, mimi na
manaibu mawaziri wangu tunahamia juma lijalo ili tukamkaribishe Mhe. Waziri
Mkuu anayehamia Septemba mwaka huu,”
alisema Mhagama.
Mhagama
amesema kuwa kila kiongozi anayehamia Dodoma inabidi awakute walio chini yake
tayari wamekwishahamia ili kumpokea, hivyo akawataka na watendaji ambao wako
chini yake watangulie kwa ajili ya kumpokea yeye na viongozi wenzake.
Aidha,
Waziri huyo amesema kwa sasa hakuna mjadala wa kuhamia Dodoma lilobaki ni
utekelezaji tu wa kuhamia Makao Makuu.
Mhagama
amesema kama kuna Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu imetenga fedha kwenye
bajeti kwa ajili ya ujenzi, shughuli hiyo ikafanyike Dodoma ambako Serikali
inahamia. Kwa kusema hivyo kadhalika na ofisi au Wizara nyingine za serikali
ambazo zimetenga fedha ya ujenzi wakajenge Dodoma.
Suala la
kuhamia Dodoma sio geni bali limekewepo kwa kipindi kirefu ila utekelzaji wake
ndio ulikuwa bado; pia katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 suala hili
lipo, alisema Mhagama na kuongeza kuwa kipindi cha nyuma Wizara saba (7)
ziliwahi kuhamia Dodoma na kwa sasa Wizara inayoshughulikia Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iko Dodoma.
Waziri
Mhagama ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuanza ujenzi wa jengo lake
mjini Dodoma na kusisitiza kuwa Wizara na Taasisi nyingine za Serikali kuiga
mfano huo kwa kujenga ofisi zao Dodoma.
“Kwa
kuwa sisi ni waratibu wa wizara zote inabidi tuunde kikosi kazi kitakachofanya
kazi ya uratibu wa kuhama kikiwa Dodoma ili kuwawezesha na watumishi wenzetu
kutekeleza agizo la Mhe. Rais la serikali nzima kuhamia huko,”alisema Mhagama.
Mhagama
amesema kuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) wameshafanya
kazi nzuri ya upimaji eneo la serikali ambalo litatumika kwa ajili ya ofisi.
“Tumefika
mwisho wa mchakato sasa ni utekelezaji na tunataka watumishi walielewe vizuri
suala hili na wawe tayari kulipokea,”alisisitiza
Mhagama.
Kuhamia
Dodoma katika kipindi hiki kunatokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alillolitoa tarehe 25 Julai, 2016
mjini Dodoma kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao ulimchagua kuwa Mwenyekiti
wa tano wa chama hicho tawala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MHAGAMA NA MANAIBU WAKE KUHAMIA DODOMA WIKI IJAYO”
Post a Comment