Saturday, August 6, 2016
TRA KUANZA KUKUSANYA KODI KWENYE NYUMBA ZA KUPANGA
Do you like this story?
MAMLAKA ya
Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza kutembelea nyumba hadi nyumba kuhakiki
gharama za upangishaji ili kukokotoa na kukusanya kodi sahihi ambayo ilikuwa
haifiki serikalini.
Hivyo,
wamewataka wananchi kutunza kumbukumbu za mikataba ya pango ili itakapohitajika
na maofisa wa mamlaka hiyo wawapatie.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana wakati akielezea kuhusu makusanyo ya kodi kwa mwezi
Julai, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo
alisema hatua hiyo ni moja ya mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Alisema
kwa Julai, TRA imekusanya Sh trilioni 1.055 sawa na asilimia 95.6 ya lengo la
kukusanya Sh trilioni 1.103 iliyopangiwa na serikali kwa mwezi huo.
Alisema
ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka jana, TRA ilikusanya Sh bilioni
914 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.43 ya makusanyo ya mwezi huu huku kwa
mwaka wa fedha 2016/2017, TRA imepewa lengo la kukusanya Sh trilioni 15.1
ikilinganishwa na lengo la mwaka jana la Sh trilioni 13.32.
“Natoa
wito kwa wapangaji na wapangishaji kujiepusha na aina yoyote ya udanganyifu
katika suala zima la kodi halisi ya pango kwa kuwa inaweza kuwasababishia
kushtakiwa endapo udanganyifu huo utabainika,” alieleza Kayombo.
Kwa sasa,
wapangaji wengi hawalipi kodi serikalini baada ya kupanga nyumba, na badala
yake wamekuwa wakilipa fedha za pango kwa wamiliki wa nyumba ambao wengi wao
pia hawalipi kodi serikalini zaidi ya kulipia kodi za majengo.
Wapangaji
wamekuwa wakilipishwa kodi ya pango kuanzia ya miezi sita hadi mwaka moja na
kodi hizo zimekuwa zikitofautiana kutokana na hadhi ya nyumba, eneo ilipo,
ukubwa wake na huduma ilizonazo kama maji na umeme.
Aidha,
Kayombo alisema pia mamlaka hiyo itatembelea waajiri katika maeneo mbalimbali
kuhakiki na kukagua usahihi wa orodha na malipo ya ajira ili kujiridhisha kama
kodi za ajira zinakokotolewa na kulipwa serikalini inavyostahili.
Alisema
mbali na mkakati huo, TRA imeweka mikakati ya kuhakikisha walipakodi wapya
wanasajiliwa zaidi pamoja na kuhuisha taarifa za walipakodi kwa kuhakikisha
Namba za Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) zisizotumika zinafutwa katika mfumo wa
mamlaka.
“Maandalizi
ya kuhuisha taarifa za walipakodi yako katika hatua za mwisho yakihusisha
upigaji picha, kuchukua alama za vidole pamoja na vielelezo muhimu vya
mlipakodi ili kuhakikisha kila biashara inakuwa na TIN moja tu yenye taarifa
sahihi na za uhakika,” alifafanua.
Alisema
TRA imeboresha mifumo yake ili kupunguza au kuondoa changamoto za kutopatikana
kwa mtandao ambayo mara nyingi huathiri makusanyo ikiwa ni pamoja na
kuunganisha mifumo ya TRA na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ili
kuhakikisha mapato ya serikali yanakusanywa kwa usahihi na wakati.
Pia
wanaendelea kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kwa kuhakikisha
wafanyabiashara wote wanaostahili kutumia mashine za kielektroniki za kodi
(EFDs) wanazitumia ipasavyo pamoja na kuwakagua wanunuzi wanapotoka madukani
kwa lengo la kuhakikisha wana risiti halali na sahihi kwa manunuzi yao.
Kayombo
alisema TRA inawaasa wananchi kuhakikisha wanakagua risiti zao za manunuzi na
kuangalia usahihi wa fedha walizolipa na uhalali wa risiti yenyewe.
“Tunatoa
wito kwa umma kutoa risiti wakati wa kuuza na kudai risiti wakati wa manunuzi
ya bidhaa au huduma kwani sheria ya fedha ya mwaka huu imerekebisha sheria ya
usimamizi wa kodi na wasiodai risiti kwa manunuzi yoyote watapata adhabu ya Sh
elfu thelathini hadi Sh milioni moja na nusu,” alisema.
Alisema
kwa sheria hiyo kutotoa risiti na kutodai ni makosa kwa mujibu wa sheria na
hatua zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kutotoa risiti au kutodai risiti
wakati wa mauzo na manunuzi.
Alisema
wanaendelea kukusanya mapato na kutoa elimu kwa wananchi hasa mabadiliko ya
sheria mbalimbali za kodi kama Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa hivi
karibuni ili kujenga uelewa na kukuza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari.
Tangu
kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, Rais John Magufuli amekuwa
akisisitiza Watanzania kujenga tabia ya kutoa na kudai risiti kwa kusisitiza
‘ukinunua dai risiti na ukiuza toa risiti.’
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TRA KUANZA KUKUSANYA KODI KWENYE NYUMBA ZA KUPANGA ”
Post a Comment