Saturday, August 6, 2016
BASI LA KISBO LAUA WATU 3 MOROGORO
Do you like this story?
WATU
watatu wamekufa papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa baada ya basi lenye
namba za usajili T 402 CRY aina ya Scania mali ya Kampuni ya Kisbo – Safari
kupinduka mkoani Morogoro. Basi hilo lilikuwa likitoka mkoani Tabora kwenda Dar
es Salaam.
Imeelezwa
kuwa basi hilo lilipinduka wakati likijaribu kukwepa gari lingine eneo la
Kwambe, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro kwenye barabara kuu ya Dodoma –
Morogoro.
Kaimu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira alisema kuwa tukio hilo
lilitokea majira ya saa 12: 30 jioni, juzi, mwaka huu eneo la Kwambe, kata ya
Dumila, tarafa ya Magole wilayani Kilosa mkoani Morogoro kwenye barabara kuu ya
Dodoma- Morogoro.
Alisema
basi hilo likiendeshwa na Davis Samora (38) mkazi wa Dar es Salaam liliacha
njia na kupinduka wakati likijaribu kukwepa gari lenye namba za usajili T957
BUV aina ya Scania lenye trela namba T 919 BVA likiendeshwa na dereva
asiyefahamika akitokea Morogoro kwenda Dodoma na ambaye alikimbia baada ya
ajali kutokea.
Kwa mujibu
wa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, dereva huyo alijaribu kuyapita
magari matatu mbele yake bila tahadhari na kusababisha ajali hiyo.
Kaimu huyo
alitaja majina ya waliokufa kuwa ni Francis Shija (70) mkazi wa Nzega, mkoa wa
Tabora, mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 45 hadi 50 ambaye
hajatambulia jina , pamoja na mtoto mdogo wa kiume ambaye bado hajatambuliwa
kwa jina na umri wake ni kati ya miaka mitatu hadi minne.
Aliwataja
majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro ni Kinazi
Machum (38), ambaye ni Mhandisi na Mkazi wa Tabora, Mathei Fidelis (30), mkazi
wa Singida na Baraka Ruta (4) mkazi wa Mwanza.
Wengine ni
Juma Bilal (30) mkazi wa Nzega, Ebebeza Richard (22) mkazi wa Mbeya, Hamis
Mogela (30) mkazi wa Nzega, Pili Waziri (44) mkazi wa Tabora na Prisca Shija
(30) mkazi wa Nzega na wote wanaendelea vyema, wakati maiti wakiwa
wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali hiyo ya Rufaa.
Kaimu
Kamanda alisema kuwa, polisi wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa ambaye ni dereva
wa gari T 957 BUV aina ya Scania lenye trela namba T 919 BVA ili aweze
kufikishwa katika vyombo vya sheria .
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ BASI LA KISBO LAUA WATU 3 MOROGORO”
Post a Comment