Friday, July 3, 2015
BIASHARA YA KADI ZA KLINIKI KWA WAJAWAZITO YASHAMIRI,ZAUZWA SH 3,000
Do you like this story?
WAKATI
Sera ya Afya nchini ya mwaka 2007, chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii, inaeleza wazi kwamba kina mama wajawazito wanaohitaji huduma
za afya katika taasisi za umma, kwa maana ya Hospitali, Vituo vya Afya na
Zahanati, pamoja na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano watapatiwa huduma
bure, hali halisi ilivyo ni tofauti kabisa katika taasisi hizo za umma nchini
Uchunguzi
wa muda sasa, uliofanywa katika maeneo kadhaa yanayotoa huduma za afya kwa kina
mama wajawazito nchini, umebaini kwamba mbali na kina mama hao kutakiwa
kuchangia huduma mbalimbali wanazotakiwa kupata kwa mujibu wa sera hiyo ya
afya, hata Kadi za Kliniki sasa wanatakiwa wazilipie kwa gharama ya kati ya Sh
2,000 hadi 3,000.
Hali
hiyo ya kugeuza maeneo ya kutolea huduma za afya ya jamii kama vitega uchumi
kwa baadhi ya watoa huduma wenye tamaa ya kipato na wasiozingatia maadili ya
kazi zao pamoja na sera nzima ya afya ya jamii, imetafsiriwa na baadhi ya
wadadisi wa mambo nchini kwamba Tanzania kwa sasa inakabiriwa na mazingira
hatari ya kuishi kwa mama na mtoto.
Sera
ya Afya ya Mama na Mtoto ya mwaka 1990, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007,
inaeleza kwamba afya ya mama na mtoto ni mfumo wa utoaji huduma maalumu kwa
wanawake walio katika umri wa uzazi na watoto wenye umri chini ya miaka mitano,
hasa watoto wachanga tangu kuzaliwa hadi siku 28.
Huduma
kwa mama na mtoto zinazotajwa na sera hiyo, zinajumuisha kutambua viashiria au
vidokezo hatari kwa wanawake na watoto, chanjo, tiba, elimu ya uzazi, uzazi
salama, mbinu shirikishi za udhibiti wa magonjwa ya watoto, afya katika jamii,
lishe na afya mashuleni.
Sera
hiyo ilitungwa mahsusi na Serikali, kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
kwa lengo la kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga, hasa
baada ya kubainika kuwepo kwa vifo vingi vya watoto wachaga ambao idadi yao
ilifikia wastani wa vifo 578 mwaka 2005, kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa
hai.
Kutokana
na hali hiyo, sera hiyo inatamka kwamba Serikali kwa kushirikiana na sekta
binafsi zinazotoa huduma bila faida pamoja na mashirika ya kimataifa,
itaendelea kutoa huduma bila malipo yoyote kwa wanawake wajawazito, watumiaji
wa huduma za uzazi wa mpango na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Hata
hivyo, pamoja na uwepo wa sera hiyo pamoja na msisitizo huo wa Serikali,
uchunguzi umebaini kwamba maeneo mengi yanayohusika na utoaji wa huduma hizo za
mama wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano, yamegeuzwa kuwa sehemu ya
biashara, kwa kina mama hao kutakiwa na baadhi ya wauguzi na wakunga kuchangia
huduma hizo kwa malipo yanayoingia mifukoni mwa watoa huduma hao.
Hospitali
ya Rufaa ya Mwananyama, katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, imetajwa
kuwa miongoni mwa taasisi za umma, ambazo wakunga na wauguzi wake wamekithiri
kwa biashara hiyo ya kadi za kliniki kwa kina mama wajawazito, ikielezwa kwamba
kina mama wengi wanaofika kwa mara ya kwanza kuanza huduma hiyo wamekuwa
watakiwa kutoa Sh 2,000 kama gharama ya kupata kadi hiyo kwa kisingizio cha
kuadimika kwa kadi hizo kunakochangiwa na bajeti finyu ya Serikali Kuu.
Mwana
mama Jorida Almasi (35), ambaye ni mmoja wa wajawazito waliokumbana na hali
hiyo alipokwenda kwa mara ya kwanza kuanza kliniki katika hospitali hiyo,
ameithibitisha kudaiwa kiasi cha Sh. 2,000 ili kupata kadi hiyo ya
kliniki, ingawa anasema hata baada ya kutoa fedha hizo hakuna stakabadhi yoyote
ya Serikali aliyopewa ili kuhalalisha uhalali wa malipo hayo.
Hali
kama hiyo ya Mwananyamala ya kugeuza biashara kadi hizo za kliniki kwa mama
wajawazito, inadaiwa kukithiri pia katika Zahanati ya Lamba, iliyoko kijiji cha
Lamba, Kata ya Mgori, Wilaya ya Singida Vijijini, Mkoa wa Singida.
Mratibu
wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika Zahanati hiyo, aliyejitambulisha kwa jina la
Zuena Mrema, amekiri kuwepo kwa tozo mbalimbali kwa mama wajawazito na wenye
watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, akidai kuwa hali hiyo inatokana na
hali halisi ya mazingira magumu yalivyo katika hospitali na vituo vya afya vya
umma, hasa katika suala zima la upatikanaji wa fedha kutoka Serikali Kuu ili
kuwawezesha kutoa huduma bure kwa mujibu wa sera hiyo.
“Hali
halisi ya mazingira magumu ya utoaji huduma kutokana na ufinyu wa bajeti
unaozikabili hospitali karibu zote za umma na vituo vya afya, hasa katika
utoaji wa huduma ya mama na mtoto, wakati mwingine tunalazimika kuwashauri kina
mama wajawazito kuja na vifaa vyao ili kuwaepushia usumbufu na ukosefu wa
huduma kwa muda muafaka,” anasema Mratibu huyo wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika
Zahanati hiyo.
Malalamiko
kama hayo ya kina mama wajawazito wanaokwenda kuanza huduma ya Kliniki kutakiwa
kulipia kadi zao, yamepokelewa kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko,
Mkoa wa Kigoma.
Mganga
Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Fadhili Suleiman, amekiri kupokea malalamiko hayo
kutoka kwa baadhi ya kina mama waliofanyiwa vitendo hivyo, huku akiahidi ofisi
yake imepanga kufanya kikao cha wafanyakazi wote wa hospitali ya wilaya hiyo
mwanzoni mwa mwezi ujao wa Julai, 2015, ili pamoja na mambo mengine, kujadili
namna ya kukomesha tabia hiyo aliyoilezea kama kero kubwa kwa kina mama na
watoto wanaostahili kupata huduma zao bure kwa mujibu wa maelekezo ya sera ya
afya nchini.
Uchunguzi
zaidi wa timu ya waadishi wetu walioko katika maeneo mbalimbali nchini umebaini
kuwepo kwa biashara hiyo ya kadi za kliniki pamoja na uchangiaji wa huduma kwa
mama wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano katika Hospitali Kuu za
Wilaya ya Nachingwea, Lindi, pamoja na Bunda, Butiama na Musoma Mjini katika
mkoa wa Mara.
Vyanzo
kadhaa vya taarifa hizi kutoka katika maeneo hayo vimethibitisha pasipo na
shaka yoyote kwamba katika baadhi ya hospitali hizo, kadi hizo za kliniki
zimekuwa zikiuzwa hadi Sh 3,000 kwa mama mjamzito anayezihitaji kutokana na
ulazima wake katika kutunza kumbukumbu za mwenendo wa ujauzito wake pamoja na
afya yake kwa ujumla.
“Hivi
ni lini hasa sisi kina wajawazito hapa nchini tutakuja kupata huduma bora za
kliniki bila malipo kama Serikali yetu inavyoagiza kila siku? Ni nani hasa
anastahili kuwajibika katika hili, ni hawa watoa huduma wetu katika vituo vya
afya au ni uongozi wa Manispaa ya Kinondoni unaopaswa kusimamia utoaji wa
huduma za afya kwa jamii katika wilaya hii?” alihoji mwana mama mmoja
aliyejitambulisha kwa jina moja la Asia, mkazi wa Mbezi Makabe, jijini Dar es
Salaam katika malalamiko yake kuhusiana na suala hilo.
Kumbukumbu
kuhusu dhana nzima ya Uzazi Salama au Usio Salama kutoka Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii nchini, zinaonyesha kwamba dhana hiyo inahitaji usimamizi wa
karibu wa mtoa huduma a afya ya ujauzito kwa mama mjamzito, kuanzia pale
inapothibitishwa kuwepo kwa ujauzito hadi wakati wa kijifungua na hata baada ya
kipindi cha wiki sita za baada ya kujifungua.
CHANZO:FikraPevu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ BIASHARA YA KADI ZA KLINIKI KWA WAJAWAZITO YASHAMIRI,ZAUZWA SH 3,000”
Post a Comment