Tuesday, August 2, 2016

WATU 14 WAPOTEZA MAISHA BAADA YA KULA CHAKULA KILICHO NA KIASI CHA SUMU.




Imeelezwa kuwa kutokana na kutokuwepo kwa uhifadhi mzuri wa chakula umesababisha watu 14 kupoteza maisha kula chakula kilicho na kiasi kikubwa cha Sumukuvu zilizokuwa katika chakula wanachotumia.

Akielezea taarifa ya vifo vya watu hao, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema vifo vya watu hao vimetokea baada ya kuibuka kwa ugonjwa usiofahamika katika Wilaya ya Chemba, Dodoma na Manyara na watu 54 waliupata ugonjwa huo na watu 14 kupoteza maisha.

Waziri Ummy alisema dalili za ugonjwa huo zilikuwa ni kuuma tumbo, kuharisha, kutapika, tumbo kuvimba na sehemu mbalimbali za mwili kuwa na rangi ya njano dalili ambazo ni za kuwa na ugonjwa wa ini.

“Ugonjwa huu umeua watu wengi hata kipindupindu hakijafikia maana kimeua asilimia 25 ya wagonjwa walioupata, hii ni changamoto kubwa na serikali inachukua hatua madhubuti kuhakikisha unathibitiwa,” alisema Waziri Ummy.

Alisema baada ya athari hizo, serikali kwa kushirikiana na mashirika ya ndani na nje ya nchi walifanya uchunguzi wa vyakula ambavyo vinatumiwa na wananchi wa maeneo yaliyoathiriwa na baada ya kukamilika kwa uchunguzi kulionekana kuwepo kwa kiasi kikubwa cha Sumukuvu katika chakula hicho.

“Kikawaida inatakiwa kuwa microgram 5 katika kila kilo moja ya chakula lakini uchunguzi ulionyesha kuwa katika kilo moja kuna microgram 5.7 hadi 204.5 na kama chakula kikiwa sumukuvu nyingi inasabisha kupata ugonjwa wa ini,” alisema Ummy.

Aidha alisema tayari serikali imeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuitaka TFDA kufanya uchunguzi wa chakula katika wilaya 10 za maeneo ambayo yanaonekana kupata ugonjwa huo pamoja na kushirikiana na wizara ya kilimo na mifugo kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kuhifadhi chakula.

Pia Waziri Ummy alitoa taarifa ya ugonjwa wa Kipindupindu na kueleza kuwa Manispaa ya Temeke imeripoti wagonjwa wanne wapya wa kipindupindu tangu Mei, 19 na hivyo kufikisha idadi ya wagonjwa 44 nchi nzima na hivyo kutahadharisha wananchi kuwa makini kwani ugonjwa huo bado upo.

0 Responses to “ WATU 14 WAPOTEZA MAISHA BAADA YA KULA CHAKULA KILICHO NA KIASI CHA SUMU.”

Post a Comment

More to Read