Tuesday, August 2, 2016

MAKUBWA: MWENYEKITI WA KIJIJI WILAYANI SHINYANGA AFUNGISHA NDOA YA MWANAFUNZI




Shirika lisilo la kiserikali la Agape linalopinga ndoa na mimba za utotoni limefanikiwa kuzuia ndoa ya binti wa miaka 16 iliyofungishwa na mwenyekiti wa kijiji cha Shabuluba wilayani Shinyanga

John Myola ni mkurugenzi wa shirika la Agape amesema shirika lake limefanya jitihada za makusudi za kuhakikisha linapinga ndoa za utotoni lakini anakosa ushirikiano kwa viongozi wa vitongoji

Aidha mkurugenzi huyo amesema pamoja na jitihada wanazozifanya lakini viongozi wa kata wamenyamaza kimya na wengine kuhudhuria kwenye sherehe hiyo
Binti huyo alikuwa akifungishwa ndoa ya kimila na kijana kutoka kijiji cha Iyombo wilayani Uyui mkoani Tabora, Masumbuko Jineneko (19) aliyekuwa ametoa mahari ya ng’ombe 15,dume watatu na jike 12 na pesa taslimu 100,000/= sawa na ng’ombe 16.

Sherehe za harusi zilikuwa zinafanyika kitongoji cha Uswahilini kijiji cha Chabuluba kata ya Usanda wilayani Shinyanga na ndoa hiyo inadaiwa kusimamiwa na baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo diwani wa kata ya Usanda (CCM) na mtendaji wa kijiji cha Shabuluba.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amesema watuhumiwa wote wawili bibi na bwana harusi walikamatwa wakiwa katikati ya sherehe za harusi na kueleza kuwa ni kinyume cha sheria za nchi kwa vile muolewaji ni mwanafunzi wa shule na aliyestahili kuendelea na masomo yake badala ya kuozeshwa.


“Tunaendelea na msako wa kuwatafuta viongozi wanaotuhumiwa kushiriki katika tukio hilo kwani wazazi na bibi harusi,viongozi wa serikali ya kijiji akiwemo diwani wa kata ya Usanda,mtendaji wa kijiji cha Shabuluba na wageni wengine walikimbia na kutokomea kusikojulikana”,alieleza kamanda Muliro.


“Inasemekana kuwa mtuhumiwa tangu achaguliwe mwaka jana kujiunga na shule ya sekondari Usanda hajawahi kuripoti shuleni hapo ambapo kwa maelezo yake anakiri kutokuripoti shuleni na wazazi wake walimkataza kwenda kuripoti shule na inaelezwa kuwa watuhumiwa hawajawahi kukutana kimwili na mtuhumiwa wa kike amepelekwa hospitali ili kupata majibu ya kitaalam kama alishawahi kuingiliwa kimwili”,aliongeza Muliro.

0 Responses to “ MAKUBWA: MWENYEKITI WA KIJIJI WILAYANI SHINYANGA AFUNGISHA NDOA YA MWANAFUNZI”

Post a Comment

More to Read