Sunday, November 27, 2016
KUFUATIA AGIZO LA WAZIRI WA ELIMU WANAFUNZI IFM WAVULIWA MAJOHO KATIKATI YA MAHAFALI
Do you like this story?
Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kimeanza utekelezaji wa agizo la
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako, kwa kuwazuia wahitimu wa ngazi ya cheti na stashahada kuvaa majoho
na kofia wakati wa mahafali yao.
Kitendo hicho kilitokea katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam
juzi baada ya mratibu wa mahafali ya 42 ya IFM, Dk. Godwin Kaganda, kutangaza
utaratibu huo licha ya wahitimu wao kuvaa majoho yao.
Dk. Kaganda alisema utaratibu huo ni kwa mujibu ya miongozo
iliyotolewa na Serikali kuhusu uvaaji wa majoho, ambao unataka yavaliwe na
wahitimu wa kuanzia ngazi ya shahada na kuendelea.
“Wahitimu wote wa ngazi ya cheti na stashahada hamtovaa majoho
wala kofia pamoja na kwamba mlishapewa awali, tunaomba radhi kwa sababu ndiyo
miongozo tuliyopewa,” alisema Dk. Kaganda.
Wiki iliyopita, Profesa Ndalichako alipokuwa akiwatunuku
vyeti wahitimu wa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa njia ya masafa,
iliyotolewa na Wakala wa Usimamizi na Uongozi wa Elimu (ADEM) mkoani Mbeya,
alisema kumekuwa na matumizi holela ya majoho suala linaloshusha hadhi yake na
kuagiza yavaliwe kuanzia ngazi ya shahada.
“Siku hizi hata mwanafunzi akimaliza chekechea anavalishwa joho.
Nafikiri haya majoho yangebaki kwa wanaohitimu digrii peke yake, ili hawa
wengine nao watamani kufika ngazi hiyo na si kila mtu anavaa,” alisema Profesa
Ndalichako.
Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 2,857 wa ngazi za cheti,
stashahada, shahada, stashahada ya uzamili na shahada ya uzamili walihitimu
masomo yao.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mwenyekiti wa Baraza la IFM,
Profesa Letisi Rutashoga, alielezea changamoto katika utekelezaji wa mpango wa
muda mrefu wa chuo hicho, ikiwamo kupanua miundombinu na utoaji wa taaluma.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni uhaba wa fedha za kuanza mradi
wa ujenzi wa kampasi mpya ya Msata iliyopo Bagamoyo na kuiomba Serikali
kuupangia Sh bilioni 2.5 katika mwaka ujao wa fedha.
Pia aliomba kuyafanyia kazi mapendekezo ya kubadilisha sheria
namba 3 ya mwaka 1972 iliyoanzisha chuo hicho, ili iweze kuendana na malengo ya
sasa ya uendelezaji wa chuo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ KUFUATIA AGIZO LA WAZIRI WA ELIMU WANAFUNZI IFM WAVULIWA MAJOHO KATIKATI YA MAHAFALI”
Post a Comment