Monday, November 14, 2016

MATANGAZO YA TIBA ASILI YAPIGWA MARUFUKU ZANZIBAR




Baraza la Tiba Asili Zanzibar, limepiga marufuku utoaji wa matangazo na vipindi katika vyombo vya habari vinavyohusu tiba asili bila kuwa na kibali kutoka katika baraza hilo.

Akizungumza katika kikao maalum kati ya viongozi wa baraza hilo na watabibu wanaotoa huduma za tiba asili na tiba mbadala, Mwenyekiti wa baraza hilo, Mohammed Kheir Mtumwa, alisema kutokana na utoaji wa matangazo na vipindi katika vyombo vya habari bila kufuata kanuni zilizowekwa na baraza na kuipotosha jamii, baraza limepiga marufuku utaratibu huo.
 
Alisema huduma za tiba asili na tiba mbadala ni huduma zinazotambulika na serikali na huduma hiyo ina thamani kubwa, lakini zimekuwa na changamoto kadhaa ikiwamo kuwapo kwa watoa huduma wasiozingatia sheria, kanuni na miongozo. Miongoni mwa changamoto hizo kwa mujibu wa Mtumwa, ni kutoa huduma bila kusajiliwa.
 
Aidha, alisema Wizara ya Afya kupitia baraza la tiba asili na tiba mbadala inakusudia kufanya mabadiliko ya sheria ili kuongeza kiwango cha adhabu kwa watakaokiuka kanuni na taratibu za chombo hicho. Alisema hivi sasa ni marufuku kwa mtu yeyote kutoa huduma za tiba asili na tiba mbadala bila ya kusajiliwa.
 
Alisema pia hairuhusiwi kuuza au kugawa dawa yoyote ya tiba asili au tiba mbadala mpaka iwe imesajiliwa na kuchunguzwa na maabara ya mkemia mkuu wa serikali kuwa ni salama au kupewa kibali na bodi ya chakula, dawa na vipodozi.
 
“Wizara ya Afya pia inapiga marufuku kwa mtu binafsi au taasisi yoyote kutumia kifaa tiba chochote kama Quantum Magnetic analyses bila kukisajili ZFDB au sehemu husika ya usajili wa vifaa tiba,” alisema.
 
Hata hivyo, alisema kuboreshwa kwa tiba asili hakutosaidia kuboresha afya za wananchi pekee, bali Zanzibar itaweza kuuza dawa na huduma hizo nje ya nchi na kupata fedha za kigeni na kuboresha uchumi wake

0 Responses to “MATANGAZO YA TIBA ASILI YAPIGWA MARUFUKU ZANZIBAR”

Post a Comment

More to Read