Saturday, November 19, 2016

POLISI YAONGEZA MUDA WA ZOEZI LA UHAKIKI WA SILAHA ZA KIRAIA KWA NCHI NZIMA




Jeshi la Polisi limeongeza muda wa huruma kwa wamiliki wa silaha walioshindwa kuhakiki silaha zao katika zoezi la uhakiki wa silaha za kiraia Tanzania Bara lililoanza Machi 22 na kumalizika Juni 30, 2016.

Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai CP Robert Boaz, amesema licha ya Jeshi la Polisi kuongeza muda wa uhakiki hadi mwezi Oktoba mwaka huu, bado wamiliki wengi hawakujitokeza kuhakiki silaha zao.

“Katika kipindi cha kuanzia tarehe 22 Machi, 2016 hadi Juni 30 serikali ilianza kufanya zoezi la uhakiki wa silaha zote za kiraia hapa Tanzania Bara, kutokana na sababu mbalimbali tuliongeza muda lakini bado baadhi ya watu hawakujitokeza,” amesema.

Amesema baada ya zoezi la awali kukamilika, tathmini inaonyesha kuwa asilimia 59.18 ya silaha zote zilizosajiliwa ndizo zilizohakikiwa na kwamba asilimia 40.82 hazijahakikiwa.

CP Boaz amesema polisi imeongeza muda wa mwezi mmoja ili wasio hakiki silaha zao wahakiki, na kwamba muda huo ni wa mwisho hautaongezwa tena.

“Tunatoa tena muda wa huruma tunawataka wamiliki wajitoekeze vituoni kuhakiki silaha zao ndani ya mwezi mmoja kuanzia Novemba 21 hadi Disemba 20, 2016. Huu ni muda wa mwisho na utakapomalizika tutachukua hatua kali.

Amezitaja baadhi ya hatua zitakazochukuliwa ikiwa ni pamoja na kufuta leseni za umiliki kwa silaha zote zisizohakikiwa, kuwatangaza wamiliki wote wa silaha kwenye vyombo vya habari walioshindwa kuhakiki pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Ametoa wito kwa wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha silaha zao katika vituo vya polisi au ofisi za serikali za mitaa na kwamba atakae tumia kipindi hiki hawatachukuliwa hatua za kisheria.

0 Responses to “POLISI YAONGEZA MUDA WA ZOEZI LA UHAKIKI WA SILAHA ZA KIRAIA KWA NCHI NZIMA”

Post a Comment

More to Read