Monday, November 21, 2016
RAIS MAGUFULI AKUTANA NA KIONGOZI WA JESHI LA UKOMBOZI LA CHINA
Do you like this story?
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 21 Novemba, 2016 amekutana na
kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni Kuu ya Ulinzi ya Jeshi la
Ukombozi la Watu wa China (PLA) Jenerali Fan Changlong, Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Viongozi hao wamezungumzia uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na China katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika masuala ya ulinzi ambapo Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) limekuwa na ushirikiano na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA)
Rais
Magufuli amemueleza Jenerali Fan Changlong kuwa Tanzania inathamini ushirikiano
huo ambao umechangia kufanikisha juhudi za kuimarisha JWTZ zinazolenga kuwa na
Jeshi la Kisasa na vifaa bora.
Dkt.
Magufuli amemuomba Jenerali Fan Changlong afikishe salamu na shukrani zake kwa
Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping na kumhakikishia kuwa Tanzania
itaendelea kushirikiana na China katika kuimarisha majeshi ya ulinzi na pia
katika masuala mengine ya maendeleo ya kijamii.
“Nimefurahishwa
na ziara yako hapa nchini kwetu, ujio wako unazidi kuimarisha uhusiano na
ushirikiano kati ya nchi zetu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa haya Hayati
Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Mwenyekiti Mao Tse-tung wa
China.
“Naomba
unipelekee salamu zangu kwa Rais Xi Jinping na umwambie kuwa pamoja na
kuendeleza uhusiano na ushirikiano wetu katika kuimarisha majeshi pia
tunatarajia kuona China inakuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi zetu
za maendeleo kwa kujenga viwanda na kushiriki katika miradi mingine ukiwemo
ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani Standard Gauge” amesema
Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Jenerali Fan Changlong amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi imara
aliouonesha katika Awamu ya Tano na amemhakikishia kuwa China itaendeleza na
kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika masuala ya usalama hasa
kuimarisha JWTZ.
Jenerali
Fan Changlong amesema Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China na Jeshi la
Wananchi Tanzania yana uhusiano wenye manufaa makubwa na kwamba hivi sasa
yanafanya uboreshaji utakaoyaimarisha zaidi na kuwa majeshi ya kisasa.
Mazungumzo
hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali
Davis Mwamunyange na Makamanda wa Majeshi wa Tanzania na China.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
21
Novemba, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ RAIS MAGUFULI AKUTANA NA KIONGOZI WA JESHI LA UKOMBOZI LA CHINA”
Post a Comment