Sunday, November 20, 2016
TANESCO WAMJIBU WAZIRI MUHONGO
Do you like this story?
SIKU
chache baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kueleza
kiu ya serikali ya kuona nchi inaondokana na mgawo wa umeme, kudhibiti
kukatikakatika kwa umeme, kuzalisha umeme wa uhakika na unaotabirika kwa
maendeleo ya viwanda, lakini pia kuwa na umeme nafuu, Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) limekuja na majibu ya hoja hizo, huku likisisitiza kuwa umeme
utapanda kwa wateja wa kati na si wa chini.
Majibu
hayo yalitolewa juzi usiku kwenye kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa hewani
na Kituo cha televisheni cha ITV na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Felchesmi
Mramba, huku akishuhudiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati
na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi, aliyetoa pia ufafanuzi wa masuala kadhaa.
Hatua
hiyo imekuja ikiwa ni wiki moja kupita tangu Ewura ilipopokea maombi kutoka
Tanesco ya kutaka kuongeza bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 18.19 kwa mwaka
2017.
Katika
maelezo yake ya juzi usiku, Mramba alisema kutokana na shirika hilo kuwajali
wateja wa kipato cha chini, wateja hao hawataathirika na mapendekezo ya bei
mpya, na badala yake watabakia na bei iliyopo sasa.
Mkurugenzi
huyo pia alisisitiza kuwa shirika hilo halina mpango wa kurudisha tozo ya
kuunganishiwa umeme ya Sh 5,000 na gharama ya huduma kwa kila mwezi ya Sh 5,520
ambazo ziliondolewa mwezi Aprili mwaka huu. Mapendekezo ya kupandisha bei ya
umeme
Akifafanua
mapendekezo hayo, Mramba alisema bei za umeme zinazotumika, zinatakiwa kutumika
hadi Desemba 31, mwaka huu na baada ya hapo Januari mwakani sheria inataka bei
mpya zitolewe.
Alisema
pamoja na mapendekezo hayo, walichoomba ni kuongezeka kwa bei kidogo ambayo
haiwezi kuwaumiza wananchi, bali itaboresha zaidi huduma na kufanya wazipate
kwa uhakika kama alivyoagiza Waziri Muhongo.
“Tanesco
ilitakiwa kufanya tathmini ya gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji
umeme na kupeleka mapendekezo hayo Ewura, ili kupitiwa na wadau, sasa suala la
kupanda au kushuka kwa bei itategemea na mapitio ya tathmini ya gharama za
kuzalisha, kusafirisha na kusambaza tulizowasilisha Ewura,” alisema Mramba.
Akizungumzia
kuhusu kuondolewa kwa tozo ya gharama za kila mwezi pamoja na tozo ya
kuunganishiwa umeme kwa wateja wapya, Mramba alisema katika mapendekezo hayo
tozo hizo hazipo na wala hawana mpango wa kuzirudisha na kwamba wateja wa chini
wao wataendelea kununua umeme kwa bei iliyopo sasa.
“Tulishaziondoa
ili wananchi waweze kupata umeme kwa bei nafuu na hatuna mpango wa kuzirudisha
kwa sasa na hata katika mapendekezo yetu wateja wa kima cha chini wao
hawataathirika, tunawajali wataendelea na bei ya sasa,” alisema Mramba.
Alisema
kilichofanyika ni mabadiliko kidogo hasa kwa wateja wa kati na wengine ambao
wamependekeza bei ipande kidogo ili waweze kutoa huduma bora zaidi kama
inavyotakiwa.
Umeme
wa viwanda Akizungumzia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania
kuwa nchi ya viwanda, Mramba alisema hadi sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazotoza gharama ndogo za umeme wa viwandani.
Alisema
hivi sasa tozo za umeme wa viwandani nchini ni kiwango cha senti 6.9 ya dola za
Kimarekani kwa uniti moja, wakati nchi nyingine za Afrika Mashariki tozo zipo
juu.
Akifafanua
hilo Mramba alisema Rwanda wanatoza uniti moja ya umeme wa viwandani kwa senti
23 za Dola za Kimarekani, Kenya na Burundi wanatoza senti 8, huku Uganda
wakitoza senti 12 za Dola za Kimarekani kwa uniti moja.
Akizungumzia
mapendekezo yaliyowasilishwa Ewura, Mramba alisema wameomba tozo ya viwanda
iongezeke kutoka senti 6.9 hadi 8 bei ambayo hata hivyo bado itakuwa chini
ukilinganisha na tozo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki ukiondoa Kenya na
Burundi.
“Pamoja
na kupendekeza kuongezeka kwa tozo ya umeme wa viwandani kutoka senti 6.9 hadi
8, bado Tanzania itakuwa nchi inayotoza gharama kidogo na hii itawezesha nchi
kuelekea kwenye uchumi wa viwanda,” alisema Mramba.
Aidha
alisema katika mapendekezo hayo waliwasilisha kutofautisha wateja baina ya
wateja wadogo wa nyumbani na wateja wa viwanda vidogovidogo ambapo awali wote
walikuwa kwenye kundi moja.
“Tumewasilisha
mapendekezo ya kutenganisha wateja wadogo wa nyumbani na wale wa viwanda
vidogo, ambao awali walikuwa kwenye kundi moja, hii itasaidia kuondoa kero ya
tozo kwa wateja hao, na sasa watalipa kutokana na matumizi yao,” alisema
Mramba.
Alisema
dhana kuwa Tanesco ndiyo walioamua kuwasilisha mapendekezo ya bei ya umeme si
sahihi na kwamba bei hizo hazijaanza kutumika kwani Tanesco haina mamlaka ya
kufanya hivyo na kuongeza kuwa ombi hilo la mabadiliko ya bei limewasilishwa
kulingana na agizo la kubadilisha bei za umeme la mwaka 2016.
Katika
agizo hilo, bei hizo zilizoanza kutumika Aprili Mosi mwaka huu, zinatakiwa
kubadilika mwaka 2017 na kwa mujibu wa Sheria, Ewura iliiagiza Tanesco
iwasilishe ombi la mabadiliko ya bei ya umeme kwa mwaka 2017, ambayo ndiyo hayo
yaliyowasilishwa.
Ngamlagosi
alisema wamepokea ombi la mapendekezo ya Tanesco ya kurekebisha bei ya umeme
hadi kufikia asilimia 18.19 kwa mwaka 2017 na kwamba wajibu wao kwa mujibu wa
sheria ni kukusanya maoni ya wadau ili kupata mapendekezo yao kabla ya kutoa
uamuzi.
Ngamlagosi
alisema wamepokea mapendekezo yenye sehemu kuu tatu, moja ni kupanda kwa
asilimia 18.19, pili ni kugawanya kundi la wateja wa kawaida wa nyumbani na
pendekezo la tatu ni kuwepo kwa kundi la wafanyabiashara wadogo, wateja wa
mabango na minara ya simu ili mtumiaji mdogo wa nyumbani asiumie kwa kuwekwa
kwenye kundi la watumiaji wa umeme wa viwanda vidogo.
Alisema
Tanesco imeomba kundi hilo livunjwe kwenye makundi mawili ili kuwe na kundi la
watumiaji wa kawaida wa umeme wa nyumbani ambao awali walichanganywa na viwanda
vidogovidogo.
“Tunao
wajibu wa kuisikiliza Tanesco kama mteja wetu, na baada ya kupitia ombi lake na
kukidhi vigezo tulitangaza ombi hilo kwenye gazeti la serikali kuhusu kutoa
maoni, na tumeshafanya hivyo na tumeshakusanya maoni mengi kutoka makundi
tofauti hata wauzaji umeme wa Tanesco,” alisema Ngamlagosi.
Alisema
maombi hayo yalipokelewa Novemba 4, mwaka huu na waliyapitia na kuona yanakidhi
vigezo na wakaitisha mikutano ya wadau kutoa maoni yao kuanzia Novemba 16 na
kwamba Novemba 25, mwaka huu watafunga pazia la kupokea maoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ TANESCO WAMJIBU WAZIRI MUHONGO”
Post a Comment