Tuesday, April 15, 2014

HIZI HAPA SABABU ZINAZOWAFANYA MBEYA CITY FC KUWA BORA MSIMU HUU.






MBEYA CITY fc ni klabu ya kwanza kuipatia Azam fc ubingwa wake  wa kwanza tangu ianze kushiriki michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2008/2009.
Ardhi ya Mbeya imekuwa ya kwanza kwa Azam fc kutwaa ubingwa ndani yake.
Azam fc imekuwa klabu ya kwanza kuwafunga Mbeya City msimu huu katika uwanja wao wa nyumbani wa kumbukumbu ya Sokoine.
Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog amekuwa kocha wa kwanza kuwapatia mafanikio ya ubingwa wa ligi kuu Azam fc.
Rekodi nyingi sana zimewekwa kwa Azam fc msimu huu, lakini yote hii inatokana na ubingwa huo kuwa wa kwanza kwao.
Msimu wa mwaka huu umekuwa na ushindani mkubwa mno hasa katika nafasi ya ubingwa.
Klabu mbili kongwe za Simba na Yanga zimekumbana na changamoto kubwa kutoka kwa Azam fc na Mbeya City katika nafasi nne za juu.
Mpaka sasa kimeeleweka ambapo Yanga pekee wameweza kushika nafasi ya pili, wakati Simba wakitupwa nafasi ya nne.
Imekuwa kazi ngumu kwa wafalme hawa wa soka la Tanzania kutoka mwaka 2000 kuachia ubingwa zaidi ya kupokezana kama mbio za vijiti.
Wana TamTam Mtibwa Sugar walibeba `ndoo` mwaka 1999 na 2000, baada ya hapo Simba na Yanga walikuwa wanatawala, lakini mwaka huu 2014 wamepinduliwa rasmi kwa Azam fc kutwaa taji.
Cheche zinawaka zaidi kwa Simba kwasababu kwa misimu miwili mfululizo wanakosa michuano ya kimataifa.
Angalau Yanga mwaka huu walishiriki ligi ya mabingwa na kuonesha upinzani mkubwa, na mwakani wataiwakilisha Tanzania katika michuano ya kombe la shirikisho.
Kwa upande wa Simba imekuwa pigo kwao kwasababu mashabiki wake walizoea kuona timu yao inawakilisha bendara ya Tanzania kimataifa.
Azam fc wamestahili kutwaa ubingwa kwasababu ya uwekezaji mkubwa waliouweka katika kikosi chao kuanzia vifaa vya mazoezi na mazingira ya kambi kwa wachezaji.
Ingekuwa fedhea kwao kukosa ubingwa, kwasababu hawakustahili kushika nafasi ya pili ambayo wameshaishika sana misimu ya nyuma.

Matokeo mazuri kwao ilikuwa ni ubingwa tu na ndio maana waliweka mikakati mikubwa ya kufanya vizuri na katika mechi 25 walizocheza hawajapoteza mechi yoyote
Ukirejea kwa Mbeya City fc, hii ni klabu pekee iliyopanda ligi kuu msimu huu na kuonesha ushindani mkubwa kutoka mwanzo wa ligi mpaka sasa ligi inaelekea ukiongoni.
Wenzao Ashanti hatima yao imebakia mikononi kwa kocha wa Prisons, David Mwamwaja mnamo aprili 19 mwaka huu.
Kama watatoa sare mechi hiyo watashuka daraja, na matokoe pekee yatakayowasaidia ni kushinda tu.
Rhino Rnagers wao wameshashuka daraja mpaka sasa.
Kwa mazingira hayo, Mbeya City imekuwa timu bora zaidi msimu huu ukiangalia kigezo cha ugeni wa ligi kuu.
Huwezi kuwafananisha Mbeya City na Azam fc, Yanga, Simba, Mtibwa, Kagera Sugar, Coastal Union kwa kigezo cha ukongwe.
Wao ni wageni sana kwani ndio kwanza msimu wao wa kwanza.
Wachezaji wengi wa Mbeya City ni wageni na hawana majina kabisa katika soka la Tanzania.
Mpaka sasa wagonga nyundo hawa wa Mbeya wamecheza mechi 25 na kushinda mechi 12, sare mechi 10 na kufungwa mechi 3. Kwa matokeo hayo wamefikisha pointi 46 katika nafasi ya nne.
Hata hivyo safu yao ya ushambuliani imeweza kufunga mabao 32, huku safu ya ulinzi ikiruhusu kufungwa mabao 20.
Yanga waliwafunga Mbeya city bao 1-0 katika uwanja wa Taifa na kule Mbeya mzunguko wa kwanza walitoka sare ya bao 1-1 katika dimba la Sokoine.
Coastal Union katika mechi ya mzunguko wa kwanza walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City uwanja wa sokoine, lakini mechi ya mzunguko wa pili Mkwakwani, wagosi wakashinda mabao 2-o.
Simba waliambulia pointi moja moja kwa mechi zote mbili ambapo Mbeya walitoka sare ya 1-1 na Dar es salaam walitoka sare ya 2-2.
Azam fc katika mechi ya kwanza chamazi, walilazimisha sare ya mabao 3-3 na Mbeya wakashinda 2-1 na kutwaa kombe huko huko.
Kwa mazingira hayo, Yanga, Coastal na Azam fc ni timu pekee zilizoweza kuifunga Mbeya City.
Nini kimekuwa nyuma ya Mbeya City mpaka wanakuw ana upinzani mkubwa kiasi hicho?
Baadhi ya sababu ambazo zinawapa nguvu wagonga nyundo hawa wa Mbeya zaweza kuwa ni;
Mosi; falsafa ya kocha mkuu, Juma Mwambusi na msaidizi wake, Maka Mwalwisyi.
Makocha hawa wanaamini katika soka la vijana na kuwapa nafasi ya kucheza kwa mechi yoyote ile.
Mara nyingi Mwambusi anaeleza kuwa mchezaji yoyote unayemuona bora duniani alipewa nafasi ya kucheza na akafanikiwa kupata uzoefu mkubwa na kung`ara.
Kwa mantiki hiyo, huwa anawapa vijana wake nafasi na kukwepa kuonesha kuwa anawategemea wachezaji fulani.
Mwambusi amekuwa akichagua timu yake kwa kuangalia ufiti wa mchezaji kwa mechi fulani na anaweza kuwabadilisha anavyotaka.
Katika kikosi chake hakuna mchezaji tegemeo, na ndio maana leo hii unaweza kumuona Mwegane Yeya yuko benchi, lakini Jeremiah Peter yupo uwanjani  na anafanya kazi kubwa.
Ukiona Paul Nonga unaweza kuogoapa kuwa hawatafunga, lakini unashangaa kumuona Peter Mapunda amevaa jezi ya zambarau na kuonesha soka zuri mno.
Kwa mzingira haya, wachezaji wanajiamini na kuamini kuwa watapangwa wakati wowote, cha msingi wajitume katika mazoezi.
Kwa hili Mwambusi ameweza kuwaweka pamoja wachezaji wake na kuooneana wivu kwenye mechi.
Pili; kujielewa kwa wachezaji wa Mbeya City fc. Ni ngumu sana kugundua kuwa wachezaji wa klabu hii wapo katika dhiki fulani.
Lakini taarifa za kuaminika kutoka ndani ya timu hii ni kuwa kuna wakati wachezaji wanacheleweshewa mishahara yao na posho.
Wakati wote wamekuwa wavumilivu sana na hii inatokana na makocha wao kuwajenga katika mazingira ya kuamini kuwa Mbeya City wanapita na safari yao ni kwenda kimataifa.
Wanapenda kufanya kazi yao na ni wazalendo wakubwa mno, huku wakiamini kuwa ipi siku watauzika.
Ukiwa na wachezaji wenye malengo ya kufanya kazi kwanza na kusubiri mafanikio baadaye basi watakusaidia kama ilivyo kwa Juma Mwambusi.
Tatu; nidhamu kubwa kwa wachezaji. Vijana wa Mbeya City fc wana nidhamu nzuri uwanjani na nje ya uwanja.
Wamejengwa katika misingi ya kuheshimu miiko ya mpira, hivyo ni ngumu kuwaona wakifanya makosa ya kujirudia rudia au kufanya fujo uwanjani.
Kwa mara ya kwanza walionekana kuwa na hasira katika mechi iliyopita dhidi ya Azam fc na sababu kubwa ilikuwa ni presha ya mchezo wenyewe.
Lakini kwa takribani msimu mzima wamekuw a na nidhamu nzuri ikiwepo nidhamu ya uwanjani.
Nne; kufanikiwa kucheza kitimu; Mwambusi amefanikiwa kwa hili kama makocha wengi duniani wapendavyo.
Kuwa na timu inayocheza kitimu bila kutegemea matokoe kwa wachezaji fulani ni faida kubwa mno.
Hata timu kubwa duniani kuna wakati zinajenga matokeo yake kupitia mchezaji mmoja.
Mfano kwa muda mrefu Lionel Messi amekuwa mwamuzi wa matokoe kwa FC Barcelona pamoja na Cristiano Ronaldo kwa Real Madrid.
Wachezaji hawa wanapokabwa ile `ngado kwa ngado` basi timu nzima inapwaya.
Lakini kwa kocha Mwambusi imekuwa ni tofauti. Timu yake imekuwa ikicheza kitimu na kila anapokosekana mchezaji mmoja basi hakuna shida.
Tano; Wachezaji kuwa na nguvu za kucheza kwa dakika zote. Wanandinga wa Mbeya City wana uwezo wa kucheza kwa dakika zote na kuhimili presha ya mchezo.
Hawaishiwi na pumzi ndani ya dakika 90. Haya ni matunda ya maandalizi yao ya muda mrefu.
Wamekuwa hawatabiriki wanapokuwa uwanjani. Kwa muda wote wanacheza kwa kasi nzuri na kuilinda mpaka mwisho wa mchezo.
Pia hili limewabeba sana tofauti na timu nyingine zinazokata pumzi katika dakika fulani.
Sita; Mashabiki wengi kuwepo nyuma yao. Kwa msimu mzima mashabiki wa soka mkoani Mbeya wamekuwa nyuma ya klabu yao na wanaweza kusafiri kwenda mikoani kuishangilia timu yao.
Wameleta utamaduni mpya kwa timu za Tanzania kwani ni kawaida kuikuta Simba akicheza na Oljoro lakini mashabiki wa Arusha wanaishangilia Simba badala ya timu yao.
Kwa Mbeya imekuwa ni tafouti kabisa hata Simba na Yanga zimepoteza mashabiki wengi.
Wachezaji wanafurahi kuona mashabiki wengi wapo nyuma yao, hivyo kucheza kwa kujituma ili kuwalipa fadhila.
Mashabiki ni wachezaji wa kumi na mbili, hivyo Mbeya wamefanikiwa kwa hili na ndio sababu ya timu yao kufanya vizuri msimu huu.

Hizi si sababu pekee zilizowafanya Mbeya City fc kufika hapo walipo, bali zipo nyingine nyingi ambazo nitazieleza baadaye.

0 Responses to “HIZI HAPA SABABU ZINAZOWAFANYA MBEYA CITY FC KUWA BORA MSIMU HUU.”

Post a Comment

More to Read