Tuesday, April 15, 2014

YANGA WAKIJIANDAA KUMALIZA HASIRA KWA SIMBA, UCHAGUZI JUNI 15 MWAKA HUU!!.




YANGA wanajiandaa kufuta machungu ya kupoteza ubingwa wao msimu huu kwa wana Lambalamba Azam fc kwa kuhakikisha wanaibuka kidedea katika mchezo wa jumamosi (aprili 19) mwaka huu dhidi ya mahasimu wao wa jadi, wekundu wa Msimbazi Simba.

Yanga  wapo mjini Moshi, mkoani Kilimanajaro  na leo hii wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki na moja ya timu ya mkoani humo.

Charles Boniface Mkwasa `Master`, kocha msaidizi wa Yanga amesema malengo yao ni kuhakikisha wanawafunga Simba hata kama wameshapoteza ubingwa.

Yanga walioambula nafasi ya pili msimu huu na kuwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la shirikisho mwakani wataingia uwanjani kucheza na Simba yenye mwendo wa kusuasua msimu huu.

Hata hivyo nao Simba wamekuwa wakitamba kuwa mechi yao na Yanga watapambana kwa nguvu zote ili kuwaumiza Yanga mara mbili .

Endapo Yanga watafungwa mechi hiyo,  basi watakuwa na maumivu ya kupoteza ubingwa na kufungwa na mahasimu wao Simba sc.

Mechi ya Yanga na Simba huvuta hisia za mashabiki wa soka nchini, na hivi sasa kila kona joto limeanza kupanda.
Huwa ni raha sana kwa timu moja kuifunga timu nyingine baina ya klabu hizi kongwe nchini.
Mechi iliyopita ya ligi kuu bara Yanga walishinda mabao 2-1 dhidi ya JKT Oljoro katika dimba la Shk. Amri Abeid jijini Arusha na kufikisha pointi 55 katika nafasi ya pili, wakati Simba walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Ashanti  ndani ya uwanja wa Taifa na kubakia na pointi zao 37 katika nafasi ya nne.

Wakati timu hizi zikiwa katika maandalizi ya mechi hiyo, taarifa kutoka ndani ya klabu ya Yanga zinaeleza kuwa Kikao cha Kamati ya Utendaji kilichokaa  tarehe 10 Aprili 2014 Makao Makuu ya klabu kilikubaliana kuwa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa YANGA SC utafanyika tarehe 15 Juni 2014.

Taarifa za taratibu za Uchaguzi zitatangazwa hapo baadaye na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Mh Alex Mgogolwa.
Hii itakuwa fursa kwa wanachama wa Yanga kuomba nafasi mbalimbali klabuni hapo.
Ikumbukwe kuwa mwenyekiti wa sasa wa Yanga, Yusuf Manji alishawahi kutangaza siku za nyuma kuwa hatagombea tena nafasi hiyo.

Tamko la Manji liliwagusa wana Yanga wengi wenye mapenzi na kiongozi huyo aliyeisaidia Yanga kufika hapo ilipo.

Manji katika muda wake wa udhamini na Uongozi, amekuwa akiifanyia timu mambo makubwa ikiwemo usajili wa wachezaji ghali na kuweza kuweka kambi nje ya nchi hususani barani Ulaya.

Tusubiri kama nia yake ya kutogombea ipo palepale au atabadili maamuzi.

0 Responses to “YANGA WAKIJIANDAA KUMALIZA HASIRA KWA SIMBA, UCHAGUZI JUNI 15 MWAKA HUU!!.”

Post a Comment

More to Read