Monday, April 7, 2014

SIMBA,MBEYA CITY VITANI.




 Mbeya City wataishusha Yanga katika nafasi ya pili kama wataibuka na ushindi leo dhidi ya Ashanti United kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, huku Simba wakiwa na kibarua kizito mbele ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Mbeya City ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 45, wakati Yanga inakamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 46 na  Azam FC inayoshikilia uongozi wa ligi ikiwa na pointi pointi 53.

Endapo Mbeya City itaifunga Ashanti leo itafikisha pointi 49, hivyo kuchumpa katika nafasi ya pili na kuishusha Yanga itakayoumana na JKT Ruvu kesho katika nafasi ya tatu.

Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema hana muda wa kupoteza zaidi ya kuhakikisha anatoa adhabu kali kwa kila timu atakayokutana nayo kuanzia na Ashanti.

“Tumejizatiti kikamilifu kuhakikisha tunaibuka na ushindi katika mechi zetu  zote zilizosalia ili atakayeteleza tu basi tunyakue nafasi moja kati ya mbili za juu,” alisema Mwambusi.

Kocha wa Ashanti, Abdallah Kibadeni anaingia kwenye mchezo huo akijua wazi kipigo kitazidi kuwaweka katika hatari zaidi ya kushuka daraja msimu huu.

Kibadeni amekiri kwamba mambo yamezidi kuwa magumu na kwamba kubaki kwa timu yake katika ligi kuu kutategemea kudra za Mwenyezi Mungu.

“Kuna timu sita za majeshi ambazo hizi zote ni jamii moja hapo unategemea sisi (Ashanti) tutapona kweli? angalia kwenye msimamo juu yetu zipo JKT Mgambo, Prisons na JKT Ruvu ambazo ni rahisi kabisa kwao kubebana, sasa tutahakikisha mechi tatu zilizosalia tunashinda halafu tuone tunakuwa katika nafasi ipi,”alisema Kibadeni.

Patashika nyingine leo ni ile ya Simba itakayojitupa uwanjani kukwaana na Kagera Sugar katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Simba wanahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kulinda heshima yao baada ya kutimuliwa katika mbio za kusaka  nafasi mbili muhimu za juu, yaani ubingwa au mshindi wa pili.

Kikosi hicho cha kocha Zravko Logarusic kinakamata nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kikiwa kimejikusanyia pointi 36 kupitia mechi 23, Kagera Sugar ipo katika nafasi ya tano wakiwa na pointi 33.
Simba imeondoka na wachezaji 19,  huku ikiwaacha Amis Tambwe, Joseph Owino, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Abdulhalim Humud na Betram Mwombeki.

0 Responses to “SIMBA,MBEYA CITY VITANI.”

Post a Comment

More to Read