Friday, April 11, 2014
TFDA YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA VIPODOZI ZAIDI YA 200.
Do you like this story?
MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA)
imepiga marufuku vipodozi 222, baada ya kugundulika kuwa vina viambata vyenye
sumu.
Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Nyanda za
Juu Kusini, Rodney Alananga, alibainisha hayo alipozungumza na Tanzania Daima
kwenye ofisi za mamlaka hiyo zilizopo eneo la Uzunguni jijini hapa.
Analanga alisema kuwa vipodozi hivyo
vimepigwa marufuku baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa kimaabara ambapo
uchunguzi huo umegundua kuwepo kwa viambata 11 vyenye sumu vinavyoweza
kusababisha madhara kwa binadamu.
“Mpaka sasa tuna viambata 11 vya
kisayansi ambavyo tumevichunguza na kugundua kuwa vina madhara kwa mtumiaji.
Tumegundua karibu vipodozi 222 nchini vina viambata hivyo,’’ alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo TFDA
inadhibiti uingizwaji na usambazaji wa vipodozi hususan kwenye mipaka rasmi kwa
kuweka mawakala wa mamlaka hiyo kwa ajili ya kupima vipodozi vinavyoingizwa
kwenye mipaka hiyo.
Alisema kuwa moja ya vipodozi vyenye
sumu ambavyo ni changamoto kuvidhibiti ni mafuta ya Carolite ambayo hutumiwa na
watu wengi licha ya kuwa na madhara ambayo ni ya muda mfupi na mrefu.
Aliyataja madhara ya muda mfupi
yanayotokana na kipodozi hicho ni muwasho, kutokea kwa mabaka meusi ambapo
madhara ya muda mrefu ni kansa ya ngozi ambayo hutokea baada ya sumu
kujikusanya taratibu.
Madhara mengine ni watoto kuzaliwa
wakiwa na mtindio wa ubongo.
Analanga alitoa wito kwa wananchi na
wafanyabiashara wanaouza na kuagiza vipodozi salama pamoja na kuonana na
wataalamu wa TFDA ili kuhakiki vipodozi hivyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TFDA YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA VIPODOZI ZAIDI YA 200.”
Post a Comment