Saturday, April 12, 2014
WANANCHI WAKOSA HUDUMA ZA AFYA KISA MUUGUZI KWENDA LIKIZO.
Do you like this story?
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Bw Deodatus kinawilo |
Hii ndio Zahanati ya kijiji cha gua kata ya gua ambayo umefungwa takribani mwezi mmoja. |
WANANCHI wa Kata ya Gua iliyopo Wilayani Chunya, Mkoani Mbeya,
wameilalamikia serikali kwa kushindwa kupeleka watumishi kwenye Zahanati
ya afya hali iliyopeleka kufungwa kwa jengo hilo na wao kukosa huduma.
Zahanati hiyo imefungwa kwa zaidi ya mwezi mmoja kwa kile
kinachosemekana mkunga aliyekuwepo kwenda likizo ya mapumziko.
Wakizungumza na Fahari news Blog wakazi wa Kijiji cha Gua Kata ya
Gua, walisema huduma kwenye Zahanati hiyo ilianza kusuasua kuanzia
mwezi January mwaka huu na ulipofika mwezi February ndipo waliposhangaa kuona
jengo hilo limefungwa.
“Kipindi cha nyuma huduma ilikuwa ikitolewa kwa kusuasua,
lakini hivi karibuni ndio tumeshangaa kukuta jengo hili likiwa limefungwa
na tulipofuatilia kwenye uongozi wa serikali ya kijiji tumeambiwa kuwa
muuguzi aliyekuwepo ameenda mapumziko,”alisema Krispin Mikael mkazi wa Gua.
Amesema, awali Zahanati hiyo ilikuwa na mganga
aliyetajwa kwa jina moja la Semwenza ambaye alistaafu na kijiji kukaa zaidi ya
miaka miwili bila ya mganga hivyo kuendeshwa na mkunga tu.
Amesema, tatizo kubwa ni pale mkunga huyo anapopatwa na
matatizo pamoja na kuchukua likizo ya mapumziko hivyo jengo hilo la Zahanati
hufungwa na kumsubili mpaka siku atakapo rejea ofisini.
Amesema, katika kipindi chote hicho
wagonjwa huendelea kuteseka kwa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta
huduma na wengine huishia kwa waganga wa kienyeji.
Amesema, baadhi ya wagonjwa hukimbilia kwa waganga
wakienyeji kutibiwa ambao wengi wao hutumia ramli za uchonganishi na
kusababisha migogoro isiyokuwa na ulazima ndani ya jamii.
Aidha, jitihada za kumtafuta Mwenyekiti wa Kijiji hicho kwa
nia ya kupata maelezo ya jambo hilo ziligonga mwamba baada ya kuelezwa kuwa
kiongozi huyo alikuwa amesafiri kikazi.
Fahari News ilifanikiwa kuzungumza na Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Chunya Sophia Kumbuli ambaye aliahidi
kulifanyia kazi tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kufika kwenye eneo la tukio.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WANANCHI WAKOSA HUDUMA ZA AFYA KISA MUUGUZI KWENDA LIKIZO.”
Post a Comment