Tuesday, April 8, 2014

WAVUVI HARAMU WATIWA MBARONI NA JESHI LA POLISI MKOANI KILWA, WANNE WAHUKUMIWA MIAKA SITA JELA.




Na Abdulaziz Lindi
JESHI la Polisi mkoani Lindi, limewakamata na kuwafikisha mahakamani watu kumi na mmoja, wakiwemo wanaojihusisha na vitendo vya uvuvi haramu wa kutumia mabomu kwenye Bahari ya Hindi, na madawa ya kulevya aina ya bangi, wilayani Kilwa.

Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoani hapa, Renatha Mzinga, watuhumiwa hao wamekamatwa katika msako uliofanywa na Jeshi hilo, mwishoni mwa wiki iliyopita, uliohusisha maeneo ya kata ya Lihimalyao na kijiji cha Matapatapa, kata ya Somanga.

Mzinga amesema katika msako huo, watuhumiwa hao wamekamatwa katika msako uliofanyika Aprili 26 hadi 30 mwaka huu, na hatimae kufanikiwa kukamata vifaa mbalimbali, ikiwemo pombe haramu ya moshi aina ya Gongo na bangi.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni, Nunda Mfaume Manzi, Yusufu Said (28), Abdudia Omari, Mohamedi Abdallah (43), Isumaili Mohamedi (40), Hashimu Hassani Mfaume, Fakii Limamo na Malongo Isumaili, wakazi wa Kilindoni, Mafia mkoani Pwani.

Wengine ni, Juma Nkama, Rajabu Hashimu na Aisha Chongomo, wanadaiwa kukamatwa na lita 67.5 za pombe haramu aina ya gongo pamoja na madawa ya kulevya aina ya Bangi, na kueleza wengi waliokamatwa ni wakazi wa Jijini dar es salaam na mkoa wa Pwani.

"Wathumiwa wote tumeshawafikisha katika Mahakama ya wilaya ya Kilwa, kujibu mashitaka yanayowakabiri, ambapo ni wanne tu ndio wamekiri makosa na kuhukumiwa kifungo cha miaka sita jela kila mmoja"Alisema Mzinga.

Kamanda Mzinga amewataja waliohukumiwa kuwa ni, Nunda Mfaume, Juma Nkama, Hashimu Mfaume na Hassani Said, huku wengine wakana makosa yanayowakabiri na kupelekwa rumande baada ya kukosa wadhamni.

Mzinga alifafanua kwa kusema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na Mashua moja, Injini mbili za Boti, chupa tano zilizokuwa ndani yake na mbolea inayodaiwa kutumika kutengenezea mabomu ya kienyeji, tambi, mitungi miwili ya gesi na vioo vya kuzamia, Amesema mafanikio ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, kumechangiwa na ushirikiano mzuri kati ya Jeshi hilo na baadhi ya wananchi waliokuwa wakitoa taarifa kwao.

Kamanda huyo wa Polisi mkoani Lindi, amezidi kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo, kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa baadhi ya watu wasiohitakia mema mkoa huo, ili waweze kushuhughulikiwa mara moja.

Aidha kukamatwa kwa wavuvi hao kumeongeza idadi ya watu wapatao 16 ndani ya kipindi cha wiki tatu zilizopita, wakiwemo watano waliokamatwa maeneo ya Shuka Lindi vijijini.

0 Responses to “WAVUVI HARAMU WATIWA MBARONI NA JESHI LA POLISI MKOANI KILWA, WANNE WAHUKUMIWA MIAKA SITA JELA.”

Post a Comment

More to Read