Wednesday, April 16, 2014
YANGA INAWAZIDI SIMBA KWA KILA KITU MSIMU HUU, NINI KITATOKEA JUMAMOSI?.
Do you like this story?
SIMBA SC watakabiliana na Yanga katika
mechi ya kufunga pazia la ligi kuu soka Tanzania bara jumosi ya wiki hii kwenye
uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Timu hizi zitakutana zikiwa na
mafanikio tofuati msimu huu ambapo Yanga wameambulia nafasi ya pili, huku
Mnyama akijikongoja katika nafasi ya nne.
Simba na Yanga zinapokutana katika
mechi za ligi au mashindano mengine, wachezaji, mabenchi ya ufundi, viongozi na
mashabiki wa klabu hizi kongwe nchini wanakuwa katika presha kubwa.
Unapozungumzia historia ya soka la
Tanzania, ni dhambi kubwa kutozitaji klabu hizi mbili zenye mashabiki kila kona
ya nchi hii.
Mengi yanatokea kila mechi zao
zinapokaribia. Wachezaji mara nyingi wanasakiziwa kuuza mechi pale timu moja
inapofungwa.
Wakati mwingine inasemekana viongozi wa
timu hizi huenda kwa waganga wa kienyeji kwenda kuroga timu pinzani.
Suala la ushirikiana linazungumzwa sana
katika klabu hizi, lakini ni jambo gumu kulithibitisha kisayansi kama kweli
linafanya kazi.
Simba na Yanga zinakutana jumamosi,
huku Yanga wakiwazidi wenzao kwa kila kitu.
Yanga wamecheza mechi 25 sawa na Simba
sc, lakini wameweza kushinda mechi 16, kutoa sare 7 na kufungwa mechi 2 tu,
hivyo kufikisha pointi 55 katika nafasi ya pili.
Pia Yanga ndio klabu iliyofunga mabao
mengi zaidi mpaka sasa ambapo imetikisa nyavu za timu pinzani mara 60, lakini
wamefungwa mabao 18 na kuwa timu ya pili kufungwa mabao machache.
Mabingwa watetezi Azam fc wamefunga
mabao 50 na kufungwa mabao 15 tu, hivyo kuwa timu yenye rekodi ya kufungwa
mabao machache zaidi msimu huu.
Ukirejea kwa upande wa Simba sc, msimu
huu upepo mbaya umevuma kwa upande wao kwasababu mpaka sasa wamecheza mechi 25
na kushinda mechi 9, sare 10 na kufungwa mechi 6.
Pia Mnyama Simba amefanikiwa kufunga
mabao 40 na kuruhusu nyavu zake kuguswa
mara 26.
Kwa takwimu hizi utagundua kuwa Yanga
wamekuwa bora kwa kila kitu dhidi ya Simba sc.
Safu ya Ulinzi ya Yanga inayoongozwa na
Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadri Haroub Canavaro, Kelvin Yondani na wengineo
imekuwa bora zaidi ya Simba inayoongozwa akina William Lucian ‘Gallas’, Issa
Rashid ‘Baba Ubaya’ Joseph Owino, Donald Mosoti, Nassor Masoud ‘Chollo’ na
wengineo.
Kigezo cha pekee ni idadi ya mabao
ambayo mabeki wa timu zote wameruhusu kutikisa nyavu.
Yanga wamefungwa mara 15 na Simba mara
26, hivyo Yanga wamekuwa na beki imara zaidi ya watani zao.
Ukija safu ya ushambuliaji baina ya
timu hizi, kuna utofauti mkubwa.
Yanga wamekuwa na makali zaidi baada ya
kufunga mabao 60 mpaka sasa dhidi ya mabao 40 ya Simba sc.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga
haimtegemei mchezaji mmoja kwasababu wote Saimon Msuva, Mrisho Ngassa, Didier
Kavumbagu, Jeryson Tegete, Hussein Javu, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wanaweza
kufunga pale wanapopewa nafasi ya kucheza.
Washambuliaji wa Yanga ndio wanaoongoza
kufunga mabao mengi zaidi na kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi kuliko klabu
yoyote katika mechi moja msimu huu.
Rekodi hii waliweka baada ya kuwafunga
mabao 7-0 Ruvu Shooting ndani ya uwanja wa Taifa.
Ukija upande wa Simba, mabao mengi
yametengenezwa kupitia kwa nyota wao, Mrundi Amis Tambwe, japokuwa kuna
wachezaji wengine kama akina Zahor Pazzi, Ramadhani Singano, Haruna Chanongo
ambao wamekuwa wakifunga mara kadhaa.
Hata rekodi ya kushinda na kufungwa,
Yanga wanawazidi Simba kwasasa wamefungwa mechi mbili tu wakati Simba
wamechezea kichapo mara sita.
Kwa kuangalia takwimu hizi, unaweza
kusema Yanga wana uwezo mkubwa wa kuwafunga Simba sc jumamosi, lakini mechi ya
watani wa jadi ni kitu kingine.
Mzunguko wa kwanza, Yanga walikuwa bora
zaidi ya Simba iliyosheheni wachezaji wengi vijana chini ya aliyekuwa kocha
mkuu Abdallah Kibadeni `King Mputa`.
Kipindi cha kwanza Yanga walifunga
mabao 3-0 na kujiamini kuwa wangeweka rekodi ya kuwafunga mabao mengi Simba na
kulipa kisasi cha kuwahi kufungwa mabao 5-0.
Hata hivyo mambo yalikuwa tofauti
kipindi cha pili ambapo Simba walikuja juu na kusawazisha mabao yote matatu na
kutoa sare ya 3-3.
Haya yalikuwa moja ya matokeo ya ajabu
baina ya klabu hizi.
Baada ya mechi hiyo, timu hizi zilikutana tena desemba mwaka jana
kwenye mechi ya `Nani Mtani Jembe` na kushuhudia Yanga iliyokuwa bora ikifungwa
mabao 3-1.
Matokeo hayo yaliondoka na kocha mkuu
Ernie Brandts na msaidizi wake Fredy Minziro waliofungashiwa virago.
Kuelekea katika mechi ya jumamosi, bado
Yanga wanaonekana kuwa bora zaidi ya Simba.
Lakini Simba wameenda kuweka kambi
Zanzibar na bila shaka watarejea na nguvu ya kuwavaa watani zao wa jadi.
Mpira wa miguu huwa ni mchezo wa
hesabu, ukikosea kuzifanya basi unafungwa.
Ni kawaida kuona timu bora inafungwa na
timu ya kawaida kama ilivyotokea kwa Yanga na Mgambo au Simba na Ashanti
United.
Ukiangalia vikosi vya timu zote mbili,
Yanga wana wachezaji wakali kuliko Simba, lakini si sababu ya kusema watashinda
mechi.
Simba uliowaona katika mchezo uliopita
na Ashanti si wale utakaowaona siku ya jumamosi.
Bila shaka wataingia kwa morali kubwa
ya kutaka kushinda, na viongozi wao wamewataka wachezaji kuwafunga mahasimu wao
ili kujipunguzia maumivu.
Usije kushangaa yanatokea matokeo ambayo
watu wengi hawatarajii.
Mechi ya watani ina mambo mengi na si
rahisi kutabiri kwa kuangalia vikosi vya vyao.
Usije ukaliwa nyumba yako, Mke wako,
pesa zako kwa kuweka mzigo mezani na kutabiri matokea.
Usilete mchezo na mechi ya watani wa
jadi, huwa timu zinacheza kwa kujituma mno.
Kila la kheri Simba na Yanga katika
mechi yenu ya jumamosi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “YANGA INAWAZIDI SIMBA KWA KILA KITU MSIMU HUU, NINI KITATOKEA JUMAMOSI?.”
Post a Comment