Sunday, May 25, 2014
WEKENI MPANGO MAALUM KUMALIZA TATIZO LA MADAWATI RUKWA - MH. PINDA
Do you like this story?
WAZIRI MKUU
Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Rukwa uhakikishe unamaliza tatizo la
upungufu wa madawati ili watoto wa shule za msingi wasiendelee kukaa chini.
Ametoa agizo
hilo jana usiku (Jumamosi, Mei 24, 2014) wakati akizungumza na viongozi na
watendaji wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa huo, Ikulu
ndogo, mjini Sumbawanga.
Waziri Mkuu
amewasili mkoani Rukwa jana jioni akitokea Dodoma ambapo atamwakilisha Rais
Jakaya Kikwete kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad Nguvumali wa
Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa itakayofanyika leo (Jumapili, Mei
25, 2014) kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga.
Akifafanua
kuhusu tatizo la madawati, Waziri Mkuu alisema: “Lazima mjipange kama mkoa ili
muweze kusaidia juhudi za Serikali kupunguza tatizo la madawati kwa watoto wetu
wa shule za msingi”.
“Lazima mje
na mpango maalum… mathalani kwenye Halmashauri zenu huko, angalieni hizo mbao
zinazokamatwa. Badala ya kuziuza, hizo mbao ziende kutengeneza madawati na
yakikamilika yaamuliwe kabisa haya yanakwenda shule fulani, na utaratibu
uendelee hadi shule zimalizike,” aliongeza.
Alisema
utaratibu huo unaweza kumaliza tatizo la upungufu wa madawati kwa uhakika zaidi
kwani hata Halmashauri zinapoamua kupiga mnada mbao zilizokamatwa, fedha
inayopatikana huwa haiendi kutengeneza madawati.
Kwa mujibu wa
taarifa kutoka idara za elimu za mkoa wa Rukwa, Halmashauri tatu za wilaya za
mkoa huo ambazo ni Nkasi, Kalambo na Sumbawanga Vijijini zinakabiliwa na
upungufu wa madawati 33,799, wakati mahitaji ya madawati ni 62,118 na yaliyopo
ni 28,319. Manispaa ya Sumbawanga ilisema ina upungufu wa madawati 675 bila
kutaja yaliyopo ni mangapi wala mahitaji yake ni kiasi gani.
Akizindua
Wiki ya Elimu Kitaifa mjini Dodoma Mei 3, mwaka huu, Waziri Mkuu aliitaka
Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI ambayo inasimamia sekta ya elimu iandae
utaratibu wa kuzibana Halmashauri ziwe za mjini au vijijini kwani zote zina
uwezo wa kupunguza tatizo hilo kulingana na fursa zilizonazo. “Nasisitiza jambo
hili liwe ni ajenda ya kudumu,” alisema Waziri Mkuu.
Mei 14, 2014,
wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 30 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania
(ALAT) jijini Tanga, Waziri Mkuu aliwataka Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri
kuhakikisha wanamaliza tatizo la madawati kwani nyenzo wanazo kupitia
Halmashauri wanazoziongoza.
Mapema,
akiwasilisha taarifa ya Mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Stella
Manyanya alisema mkoa huo kupitia kamati za shule na uongozi wa kata umeweka
mkakati wa kutatua tatizo la madawati kama njia mojawapo ya kuboresha taaluma
katika mpango wa Matokeo Makubwa na ya Haraka (BRN).
Akizungumzia
kuhusu hali ya miundombinu katika Mkoa huo, Eng. Manyanya alisema kazi za
ujenzi wa barabara za mkoa huo kwa kiwango cha lami unaendelea sasa baada ya
msimu wa mvua kumalizika na baadhi ya wakandarasi kupatiwa fedha na Serikali.
Kuhusu
usanifu wa Daraja la Mto Momba lililoko mpakani mwa mikoa ya Rukwa na Mbeya,
Eng. Manyanya alimweleza Waziri Mkuu kwamba kazi hiyo imesimama kutokana na
kina cha maji kupanda licha ya kuwa ilipaswa kukamilika tangu Machi mwaka huu.
“Usanifu
ulitarajiwa kukamilika Machi 2014, lakini kutokana na kina cha maji kupanda,
uchunguzi wa matabaka ya udongo chini ya maji umeahirishwa mpaka maji
yatakapopungua,” alisema.
Hata hivyo,
Mkuu huyo wa Mkoa alisema wanatarajia kazi ya usanifu na uandaaji wa nyaraka za
zabuni utakamilika mwezi Mei mwishoni na baada ya hapo zabuni kwa ajili ya
ujenzi wa daraja hilo itatangazwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WEKENI MPANGO MAALUM KUMALIZA TATIZO LA MADAWATI RUKWA - MH. PINDA ”
Post a Comment