Thursday, June 12, 2014
CHANZO CHA UGONJWA WA AJABU KWA WASICHANA KUANGUKA SHULENI CHATAJWA
Do you like this story?
Ugonjwa wa
kuanguka na kupiga kelele unaowakumba baadhi ya wasichana katika shule
mbalimbali nchini, umetajwa kusababishwa na maambukizi ya hofu
inayosababisha mwili kupata dalili za magonjwa yasiyokuwepo.
Mtaalamu wa
saikolojia na theolojia, Mchungaji John Rowse kutoka taasisi ya The
Uhakika Christian Education Trust Fund kutoka Mbeya, alisema hayo hivi karibuni
baada ya kutembelea shule zinazopata tatizo hilo mara kwa mara na
kuzungumza na wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alisema kuna
mambo kadhaa yanayochangia kujenga hofu hiyo ambayo mwili hujitayarisha
kuambukizwa, ikiwemo vitisho vya maisha kwa wanafunzi vinavyotokana na mambo
mbalimbali kama vile ugomvi na mabadiliko ambapo miili yao inahangaika
kujihami.
Kwa mujibu wa
Mchungaji huyo, upo uwezekano kuwa baadhi ya wanaoanguka, ni wasichana
wanaonyanyaswa nyumbani, wengine wanafundishwa kujidharau na wengine
wanabaguliwa na kufanyiwa unyanyapaa shuleni.
Sababu nyingine
ya kuanguka kwa wasichana shuleni kwa mujibu wa Mchungaji Rowse, ni hofu
wanayopewa wasichana hao na waganga wa kienyeji wanaotabiri au kupiga
ramli, pamoja na wachungaji au wainjilisti wanaokemea mapepo huku
wakiwashika kichwani, begani au kwenye shingo na kuwatetemesha wasichana
hao.
Mchungaji
Rowse alisisitiza kuwa dawa pekee ya kutibu ugonjwa
huo, ni utulivu kwani wanafunzi hao hususani wasichana
huambukizana kwa hofu hivyo matibabu yake ni kupunguza hofu na mawazo.
“Hofu
hiyo kwa wasichana hao husababishwa kwa imani potofu,
waganga wa kienyeji wanaotabiri au kupiga ramli … waganga
hawa wanapenda kujenga hofu ya uchawi, ili baadaye wajidai kwamba ni wao
waliondoa laana na kuleta uponyaji.
“Dawa
ya kusaidia kuzuia matukio hayo ni kuwa na mipango ya kupunguza msongo wa
mawazo shuleni, hasa miongoni mwa wasichana,” alisema.
Mchungaji
Rowse alipendekeza machifu na waganga wa jadi wasikaribishwe
shuleni kuwaombea wasichana hao kwa kuwa watawaongezea hofu.
Pia alipendekeza
wachungaji au wainjilisti wanaopenda kushika mtu kichwani, begani au kwenye
shingo na kumtetemesha, wasikaribishwe shuleni kwa kuwa nao pia ni hatari.
“Hata
wale wanaokemea mapepo kwa sauti kubwa na wakati wakifanya hivyo hupenda
kumwangalia msichana kwa ukali jicho kwa jicho.
”Katika
mazingira hayo, watoto watapata tena hofu na
wakianguka tena watasema ni pepo, lakini sivyo. Afadhali mchungaji wa
amani, amwombee kila mwanafunzi aliyekumbwa na ugonjwa huo kwa sauti ndogo tu
na kwa upole na upendo na kumfariji na utulivu. Asitamke wazi neno lo lote juu
ya mapepo,” alisisitiza.
Alishauri kuwa
kila shule iwe na mwalimu au mshauri wa kike ambaye hatoi adhabu kwa wasichana,
atakayepaswa kujenga urafiki nao na kuwa karibu nao, ili wamwamini na
kumwelezea mateso yao ya maisha, nyumbani na shuleni.
Alisisitiza
kuwa wanafunzi wa kike wapewe nafasi za kukutana katika
vikundi, ili wajadiliane pamoja kuhusu mambo yoyote, pia
walimu wajitahidi kumpa kila msichana nafasi ya kusikilizwa.
Alitoa mfano wa
Shule ya Msingi Inyonga wilayani Mlele katika Mkoa wa Katavi, ambayo
aliitembelea na kuzungumza wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alisema baada
ya shule hiyo kuanza kutekeleza ushauri huo, Mwalimu Mkuu wa shule
hiyo, Casto Ismail, alimwambia kuwa kasi ya matukio imepungua.
“Mwalimu
Mkuu huyo alinieleza kuwa wamekuwa na mitihani ya darasa ya saba, ambao kwa
kawaida husababisha msongo wa mawazo kwa wanafunzi, lakini hakuna
mwanafunzi wa darasa ya saba hata mmoja aliyeanguka wakati huo…katika madarasa
mengine ni wachache walioanguka.
“Niliwaambia
walimu wawe na uvumulivu. Mambo yatatulia kweli baada ya mabadiliko ya imani ya
wazazi na jamii… lakini watalaamu bado wanashindwa kuelewa kwa nini hali hiyo
inakutwa sana kwa wasichana na wanawake,”
alisema Mchungaji Rowse.
Mwandishi
alifika katika Shule ya Msingi Inyonga na kuzungumza na Mwalimu Ismail, ambaye
alieleza kuwa ugonjwa huo ulidumu kwa zaidi ya
miezi sita tangu ulipowakumba wasichana wanaosoma katika shule hiyo
Novemba mwaka jana.
Alifafanua
kwamba kasi ya kuanguka kwa wasichana hao shuleni hapo
imepungua baada ya kuanza kufanyia kazi ushauri wa Mchungaji Rowse,
aliyefika shuleni hapo na kuzungumza na wanafunzi. Pia alitoa
semina kwa wanafunzi, walimu na wazazi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ CHANZO CHA UGONJWA WA AJABU KWA WASICHANA KUANGUKA SHULENI CHATAJWA ”
Post a Comment