Wednesday, June 18, 2014

SERIKALI KULIPA RIBA SH 5 BILION DENI LA MIEZI SITA




Serikali italazimika kulipa hasara ya zaidi ya Sh5.2 bilioni (Dola za Marekani milioni 3.1) ambazo ni riba ya malimbikizo ya malipo ya miezi sita kwa Kampuni ya Jacobsen Elekron AS inayotekeleza awamu ya kwanza ya mradi wa umeme wa Kinyerezi, Dar es Salaam.
imebaini kuwa kampuni hiyo ya Norway inaidai Serikali Dola 48.8 milioni (Sh80.52 bilioni), yakiwa ni malimbikizo ya malipo kuanzia Novemba mwaka jana na Mei mwaka huu.

Mbali ya hayo, kampuni hiyo ilitishia kusitisha utekelezaji wa mradi huo na kuondoa vifaa vyake kama isingelipwa walau Dola milioni 25 za Marekani (Sh41.25 bilioni) hadi Juni 15 mwaka huu.

Katika barua yake ya Juni 5, 2014 iliyosainiwa na Meneja wa Mradi wa Kinyerezi wa Jacobsen, Stein Sundbye kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kunakiliwa kwa Katibu Mkuu - Hazina na mwenzake wa Nishati na Madini, kampuni hiyo imelalamikia ucheleweshaji wa malipo hayo kinyume cha mkataba baina ya pande hizo mbili.

“Rejea barua yetu ya 23 Mei, 2014 iliyotoa ilani ya siku 14 kwamba tutasitisha kazi zetu kwa mujibu wa kipengele 41.2 cha mkataba, isipokuwa kama tutapokea malipo tunayodai ya Dola 48.8 milioni kama ankara ya madai iliyoambatanishwa hapa inavyoonyesha,” inasema sehemu ya barua hiyo na kuongeza:
“Kama tulivyoeleza ilani hii inamalizika Juni 6, 2014 wakati usitishaji wa kazi utakapoanza. Licha ya kuomba tulipwe au tuambiwe ni lini malipo hayo yatatolewa, hatujapokea majibu yoyote ya kupewa fedha zetu zote au kwa awamu kama ilivyokuwa imeahidiwa na Wizara ya Fedha katika barua yenye Kumbukumbu namba CDA.327/602/01 ya Aprili 4, 2014.
Laibuka bungeni

Juzi jioni, suala hilo liliibuliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye alisema Serikali imekuwa ikipata hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na kupanga utekelezaji wa miradi mikubwa pasipokuwa na uhakika wa fedha.
Akichangia hoja ya Bajeti ya Serikali, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema) alisema: “Wakati Serikali ikitafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, tumekuwa tukiingia kwenye madeni ya ajabu ambayo kama tungekuwa makini yangeweza kuepukwa.

“Ninao mfano halisi hapa ambao unaonyesha jinsi Serikali itakavyolazimika kulipa riba ya zaidi ya Sh5 bilioni kutokana na kushindwa kulipa fedha za Kampuni ya Jacobsen inayojenga mradi wa Kinyerezi One, hii ni aibu kubwa maana tumelimbikiza madeni ya miezi sita na wanatudai Dola za Marekani 48 milioni.”

0 Responses to “SERIKALI KULIPA RIBA SH 5 BILION DENI LA MIEZI SITA”

Post a Comment

More to Read