Monday, June 16, 2014

UNICEF TANZANIA YAWATEUA AY NA FARAJA KOTA NYALANDU KAMA MABALOZI WAO WA KUHAMASISHA UMMA JUU YA UKATILI DHIDI YA WATOTO


Faraja Kota

Ambwene Yesaya(AY)

Halmashauri ya Wilaya ya Hai yazindua kituo cha huduma jumuishi cha kushughulikia ukatili wa wanawake na watoto.UNICEF Tanzania yawateua AY na Faraja K. Nyalandu kama Mabalozi wao wakuhamasisha umma juu ya ukatili dhidi ya watoto

Hai, 16 June, 2014 –Katika kusherehekea siku ya Mtoto wa Afrika tarehe 16 Juni, Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ikishirikiana na viongozi wa serikali, UNICEF na Save the Children, imezindua Kituo cha Huduma Jumuishi, kitakachowasaidia wanawake na watoto ambao wameathiriwa na ukatili.

“Katika kituo hiki, huduma za kuwasaidia wahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na huduma za afya, msaada wa kisaikolojia, ulinzi/usalama na msaada wa kisheria vinaweza kutolewa hapo katika eneo moja ndani ya kituo cha afya zikiwa zimeratibiwa vizuri Zaidi,” alisema  Charles Pallangyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Aliongeza, “kituo hiki kitasaidia kupunguza madhara zaidi ya ukatili kwa sababu wahanga wa ukatili wataweza kupata huduma zote muhimu katika eneo moja na hawatakuwa na sababu ya kurudiarudia kuwaeleza watoa huduma mbalimbali walio katika maeneo tofauti yale mambo mabaya waliyoyapitia, au kutakiwa kwenda na kurudi kutokana na ukosefu wa uratibu na uwezo wa watendaji wa sekta mbalimbali katika kuwahudumia wahanga wa ukatili kwa ukamilifu.”
Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, Dk. Jama Gulaid, anaamini kuwa kama tukifanya kazi kwa ushirikiano na serikali na wadau wengine, tunaweza kupata suluhu katika kumaliza ukatili dhidi ya watoto. “Ukatili dhidi ya watoto uko kila mahali na hatuwezi kuendelea kuufumbia macho. Watoto wote hapa Tanzania wanahaki ya kuishi na kukua katika mazingira yasiyo na ukatili. Kama sisi sote tukifanya kazi kwa kushirikiana pamoja, sina shaka tutaweza kumaliza ukatili dhidi ya watoto.”

Katika tukio hili huko Hai, UNICEF Tanzania imemteua msanii mahiri wa bongo flava Ambwene Yessyah, anayejulikana zaidi kama AY, pamoja na aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Faraja Kotta Nyalandu kama Mabalozi wao katika ‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto.’ Wote wameahidi kusaidia kampeni ya ‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto’ na wameonyesha kuhamasishwa na heshima hii waliyopewa kutoa sauti zao kutetea ulinzi wa mtoto.

“Nimepewa heshima kubwa kwa kuteuliwa kwangu kuwa Balozi wa UNICEF Tanzania na nitajitoa katika kutumia sauti yangu na umaarufu wangu kusaidia kutokomeza ukatili dhidi ya watoto hapa Tanzania,” alisema AY alipokuwa akikubali wadhifa huo.

Kwa kuwateua AY na Faraja Kotta Nyalandu kama Mabalozi wa UNICEF Tanzania wa kampeni ya ‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto’, UNICEF inategemea kuongeza uzito na muonekano zaidi wa suala la ulinzi wa mtoto katika mijadala inayoendelea kuhusu ukatili dhidi ya watoto na kuonyesha kuwa kuna suluhisho la tatizo hili. Kama mwazo wa kazi yao katika shughuli za UNICEF Tanzania, AY na Faraja Kotta Nyalandu walitembelea Dawati la Jinsia na Watoto katika kituo cha Polisi cha Hai kuona wenyewe kazi inayofanywa kusaidia wanawake na watoto waliofanyiwa au kuathiriwa na ukatili.

Utafiti juu ya Ukatili Dhidi ya Watoto, uliozinduliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto mwaka 2011, unaonyesha mambo yanayopelekea uhatarishi wa watoto kwenye ukatili kimwili na kingono hapa Tanzania – wastani wa msichana 1 kati ya 3 na mvulana 1 kati ya 7 wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono, na zaidi ya asilimia 70 ya wasichana na wavulana wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili kabla hawajafikia umri wa miaka 18. Hata hivyo, wahanga wengi hawajamwambia mtu yeyote ukatili waliofanyiwa na ni kesi chache sana zimefikishwa polisi.

Kumekuwa na maendeleo katika kuboresha hali hii. UNICEF inasaidia serikali ya Tanzania kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii kuanzisha na kuboresha ‘mifumo ya Ulinzi wa Mtoto’  katika halmashauri 13. Katika halmashauri hizi, afya, ustawi wa jamii, polisi, sekta za elimu na mahakama, magereza, wanasheria, asasi za kiraia pamoja na mifumo ya kijamii isiyo rasmi wanaunda Timu ya Halmashauri ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto na wanashirikiana kuhakikisha kuwa kesi za ukatili wa watoto zinashughulikiwa vyema na pia wanazuia ukatili kwa kuongeza uelewa wa jamii juu ya ukatili dhidi ya watoto. Lengo la Idara ya Ustawi wa Jamii ni kupanua utaratibu wa mfumo huu katika halmashauri 30 ifikapo mwaka 2016.

0 Responses to “UNICEF TANZANIA YAWATEUA AY NA FARAJA KOTA NYALANDU KAMA MABALOZI WAO WA KUHAMASISHA UMMA JUU YA UKATILI DHIDI YA WATOTO ”

Post a Comment

More to Read