Thursday, July 31, 2014

BASI LAUA 17 KUMI NA KUMI NA MOJA WATAMBULIWA.





Watu 11 kati ya 17 waliofariki dunia papohapo katika ajali eneo la Pandambili wilayani Kongwa, Dodoma wametambuliwa na wanne kati yao tayari wamechukuliwa na ndugu zao.

Ajali iliyosababisha watu 56 kujeruhiwa vibaya. iliyahusisha magari mawili ambayo ni basi aina ya Scania mali ya Kampuni ya Morobest lililokuwa likitokea Mpwapwa kwenda Dar es Salaam, ambalo liligongana na uso kwa uso na lori lenye tela, lililokuwa limepakia shehena ya mabomba.

Ajali hiyo ambayo ilisababisha vifo vya madereva wa magari hayo, ilitokea meta chache kutoka mahali ilikotokea ajali iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma David Misime aliielezea tukio hilo lilitokea saa 2 asubuhi kuwa miongoni mwa ajali mbaya ambazo zimetokea mkoani humo katika siku za karibuni.
“Ni watu 17 ambao wamekufa hapa hapa, kati ya hao 12 ni wanaume na wanawake ni watano, majeruhi ni 56, kati yao tisa wana hali mbaya zaidi,” alisema Misime.

Hadi jana jioni maiti za watu kumi na moja walikuwa wametambuliwa na wanne kati yao walichukuliwa na ndugu zao.
Waliotambuliwa ni Gabriel Lemanya (Dereva wa lori) ambaye ni Mkazi wa Ndebwe wilaya ya Chamwino, Said Lusogo (dereva wa basi), Omari Mkubwa (kondakta wa basi) na Mikdadi Zuberi ambaye alikuwa ni utingo wa lori.
Wengine ni Justin Makasi, Gabriel Chiwipe, Marick Masawe na Melina Maliseli, Wilson Sudai (wote wakazi wa Mpwapwa) watu wawili walitambulika kwa jina moja ambao ni Christina (Mpwapwa) na Nasibu mkazi wa Kongwa.

Mashuhuda walisema Polisi wa Kituo cha Kongwa walifika katika eneo la ajali muda mfupi tu baada ya magari hayo kugongana na kwamba walisaidia kudhibiti usalama wa mali za abiria, zikiwamo simu za mkononi zaidi ya 20 ambazo zilikabidhiwa kwa uongozi wa polisi Mkoa wa Dodoma.

0 Responses to “BASI LAUA 17 KUMI NA KUMI NA MOJA WATAMBULIWA.”

Post a Comment

More to Read