Saturday, February 18, 2017

MALI ZA MAKONDA ZAMUINGIZA MATATANI,KUCHUNGUZWA NA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA


SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imesema ipo tayari kuhakiki mali za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, endapo watapokea malalamiko kutoka kwa wanaomtilia shaka.
Hivi karibuni wakati akitangaza orodha ya watu wanaotuhumiwa kuuza, kuagiza na kutumia dawa za kulevya, Makonda alijikuta akiingia katika vita ya maneno na wabunge.
Msingi wa vita yenyewe ni hatua ya baadhi ya wabunge kupinga utaratibu alioutumia Makonda kuwataja kwa majina watuhumiwa hao na hata kwenda mbali zaidi wakimtuhumu na kuhoji alikopata utajiri wa ghafla.
Hatua ya kuhoji mali za Makonda ilichochewa na kauli ya Mkuu huyo wa Mkoa ambaye alionekana kukerwa na ukosoaji wa wabunge hao na hivyo kuwatuhumu wawakilishi hao wa wananchi kulala bungeni na kuitikia kila kitu ndiyoooo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa sekretarieti Maadili ya Viongozi wa Umma, Joseph Ishengoma, alisema chombo hicho kipo tayari kufanya uhakiki endapo watapokea malalamiko rasmi kutoka kwa wananchi au wabunge waliosikika hivi karibuni wakizungumzia suala hilo bungeni.
Alisema kinachotakiwa ni kufuata utaratibu ambao ni kupeleka malalamiko kwa sekretarieti hiyo kuomba kufanyika kwa uhakiki wa mali za kiongozi huyo kutokana na tuhuma walizozitoa. Kauli hiyo ya sekretarieti imekuja ikiwa imepita takribani wiki moja sasa tangu wabunge na Makonda washambuliane kwa maneno.
Miongoni mwa wabunge walioonekana kukerwa na kauli pamoja na utaratibu alioutumia Makonda na hata kutaka naye achunguzwe ni Mbunge wa Rombo (CHADEMA), Joseph Selasini,  ambaye alikwenda mbali na kutaja mali zinazodaiwa kumilikiwa na Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akichangia taarifa za Kamati za Bunge  za Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Selasini alisema Makonda amenunua jengo (apartment) lenye thamani ya shilingi milioni 600.
“Makonda amenunua apartment pale Viva Towers kwa shilingi milioni 600, Makonda amempa mke wake gari aina ya Mercedez Benz lenye thamani ya Dola 250,000 za Marekani (shilingi milioni 550) kama zawadi ya birthday,” alisema Selasini.
Gari anayotumia Paul Makonda aina ya Lexus
Siku moja kabla ya Selasini kusema hivyo, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Rushaku (Msukuma), naye aliibuka na tuhuma nyingine nzito dhidi ya Makonda na kutaka vyombo husika vimchunguze.
 “Mheshimiwa Spika, nasimama kwa kanuni ya 68(7) kuhusu jambo lililojitokeza jana (juzi) wakati wa mjadala wa Bunge…naomba mwongozo wako.
“Mimi binafsi naunga mkono jitihada za Rais kukamata wauza dawa za kulevya, lakini dalili ya kwanza ya kuanza kumhisi mtu kama anajishughulisha na biashara ambazo hazieleweki, kwanza ni mwenendo wa mtu yeyote…si Mbunge wala si nani.
 “Anatumia Lexus ya petroli ya Sh. milioni 400, lakini imekarabatiwa ofisi (yake) ya RC Dar es Salaam kwa zaidi ya Sh. milioni 400 bila kufuata utaratibu wa manunuzi wa Serikali.
“Ana ma-V8 na Mwanza amejenga jengo la ghorofa…ni kina nani wanaotakiwa kujadiliwa na kufanyiwa uchunguzi? Na hawa Mawaziri tulionao humu kwanini wamepigwa ganzi? Utawala bora, Mambo ya Ndani na Waziri wa Sheria…kwanini mmepigwa ganzi?”
Msukuma pia alihoji anakopata fedha Makonda za kwenda Paris na Marekani na kukaa siku 21 hasa ikizingatiwa kuwa tiketi moja ni Dola za Kimarekani 14,000 huku yeye na mkewe jumla ikiwa ni dola za Kimarekani 28,000.
Paul Makonda na mkewe
Kutokana na hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Sekretarieti hiyo, Ishengoma, alisema wabunge hao baada ya kutoa malalamiko ya kutilia shaka mali za Makonda, wanatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 1,000 na kisha watapewa faili kwa ajili ya kuangalia na kujiridhisha mali ambazo Makonda alizitaja kwao.
Alisema na hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.
Alisema kwa kuzingatia Katiba na sheria hiyo, Sekretarieti itakuwa na wajibu wa kupokea hati za tamko rasmi zinazohitajika kutolewa na viongozi wa umma kwa mujibu wa Katiba au sheria nyingine yoyote.
Alisema kifungu cha 18 (b) kinaeleza kuwa; Sekretarieti itapokea malalamiko na taarifa za ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma kutoka kwa wananchi.
Kifungu cha 18 (c) Sekretarieti itachunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa sheria ya maadili ya viongozi wa umma na viongozi wote wa umma wanaopaswa kuwajibika chini ya sheria hiyo.
Alisema pia sekretarieti katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa vipengele hivyo, itakuwa na mamlaka  ya kupokea na kusikiliza malalamiko yote kuhusu kiongozi yeyote wa umma yawe kwa mdomo au kwa maandishi kutoka kwa si tu wabunge hao bali kwa mwananchi yeyote bila kuuliza majina na anwani za watu waliopeleka malalamiko hayo.
Kwa mujibu  wa sheria ya maadili ya mwaka 1995 (23) (1) endapo mtu mwenye wadhifa wa waziri au wa mkuu wa mkoa amekiuka miiko hiyo, malalamiko yanaweza kuwasilishwa kwa rais na mtu yeyote kwa maandishi yaliyotiwa saini, anwani na jina la mlalamikaji.
Zaidi, Ishengoma alisema taarifa ya mali za Makonda pamoja na viongozi wengine ziliwasilishwa katika ofisi yao Desemba 31, mwaka jana kwa mujibu wa sheria. Alisema pamoja na hayo hatamzuia mtu kupeleka kile anachokijua ili waweze kufanyia kazi.
“Sheria hii yenyewe inampa mtu ‘Consumption’ kama Kamishna wa Tume ya Maadili ataangalia kama mali zake zina ushahidi na ofisi inaweza kufanya uhakiki wa kupata taarifa sahihi kama alificha hizo mali hapo awali au la na hatua ya kwanza atapewa kubadilisha.
“Na kama Kamishna akiridhia kuwa amedanganya basi atapelekwa katika Baraza la Maadili na anayelalamika  anakuwa ni miongoni mwa mashahidi na kitakachofuata atajitetea na chombo hicho kitatoa mapendekezo,” alisema Ishengoma.
SELASINI ANENA TENA
Akizungumza kwa njia ya simu jana iwapo atapeleka malalamiko katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutaka kuhakiki mali za Makonda kama alivyomtuhumu bungeni, Selasini ambaye yupo jimboni kwake Rombo alisema hawezi kupeleka malalamiko kwa kuwa viongozi wengi ni waongo.
Katika hilo wao wamekwishataja na kilichobaki ni vyombo vya uchunguzi kufanya kazi hiyo.
“Watu wamejaza mali zao majina ya shemeji zao, wake zao, watoto wao, mahawara zao hivyo kupeleka malalamiko sisi ni kujidanganya tu.
“Sisi tumeshasema na si lazima tupeleke malalamiko, hapa kinachotakiwa ni vyombo vya uchunguzi vifanye kazi zake, kwani havina watu wa kuchunguza kuanzia safari ya Ufaransa siku 21 kwa kwenda Airport kuchunguza alivyoondoka,” alihoji Selasini.
Alisema hakuna haja ya vyombo vya uchunguzi kutupia aliouita mzigo kwa watu wengine huku akisema endapo atapeleka malalamiko shahidi atatakiwa awe yeye mwenyewe na hana muda wa kupoteza katika hilo.
Alisema siku ambayo alimtuhumu Makonda kumiliki mali hizo alipomaliza tu na kutoka alifuatwa na mtu aliyemtaja kuwa wa usalama na kumweleza kuwa Makonda Dodoma ana viwanja 19 na vipo kwa jina lake.
“Hilo nalo watataka tupeleke malalamiko, hapana wanatakiwa kufika tu Ardhi Dodoma na kuangalia jinsi ambavyo alivyoviandikisha vyote kwa majina yake, lakini kwa kupeleka malalamiko hatutafika katika hili na hutampata mtu, vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake tu,” alisema Selasini.
Alisema kuundwa kwa chombo hicho lengo lake ni kuwa na viongozi wenye maadili hivyo kama watashindwa kufanya hivyo itakuwa ni kwa sababu ya kuingia katika siasa.
MSUKUMA
Alipotafutwa Msukuma kuelezea kama ana nia ya kupeleka malalamiko, alisema hiyo si kazi yake.
“Hizo ni kazi za Spika wa Bunge yeye ndiye anatakiwa kunipigia simu na kuniambia nipeleke malalamiko au wanipe maelekezo nifanye hivyo na si mwandishi,” alisema na kukata simu ghafla.
HT: MTANZANIA

0 Responses to “MALI ZA MAKONDA ZAMUINGIZA MATATANI,KUCHUNGUZWA NA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA ”

Post a Comment

More to Read