Wednesday, July 23, 2014

HAWZAT IMAM SWADIQ KUONGOZA MAANDAMANO YA KULAANI MAUAJI YA HUKO GAZA.





TAASISI ya  Hawzat Imam Swadiq wameandaa maandamano ya kulaani mashambulizi yanayofanywa na Vikosi vya Israel dhidi ya wananchi wa Palestina wasio na hatia.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Taasisi hiyo Profesa Abdul Shariff, maandamano hayo yanalenga kuueleza ulimwengu kuwa wananchi wa Tanzania wanalaani mauaji yanayoendelea huko Gaza Palestina.

Amesema kuwa maandamano hayo  ambayo yatafanyika siku ya Ijumaa  Julai 25 mwaka huu yanatarajia kuanzia Kituo cha Daladala cha Boma na kuishia Kigogo uwanja wa Bibo.

Profesa Shariff ameongeza kuwa wameamua kupaza sauti zao kulaani baada ya kuona Jumuiya mbalimbali za Kimataifa ikiwa imenyamaza huku mamia ya watu wakizi kupoteza maisha yao.

Amesema kuwa inasikitisha kuona hata vyombo vya habari hasa vya Magharibi havitoi nafasi kubwa kwa mauaji hayo ukilinganisha na mauaji yaliyotokea kwa kulipuliwa kwa ndege Malyasia.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Sheikh Hamed Jalala amesema kuwa wamealika viongozi na Mabalozi wa Nchi mbalimbali ili nao waweze kushiriki katika  kupaza sauti zao pamoja na watanzania kulaani vitendo vinavyofanywa na Israel vya kuua watu wasio na hatia.

Sheikh Jalala amesema kuwa kunyamazia tatizo hilo ni kufanya kosa kwani hakuna hata dini moja inaruhusu mauaji ya binadamu mwingine.

Amesema kuwa maandamano  hayo yatahusisha watu wa dini zote na yamepata Kibali cha Mamlaka husika.

0 Responses to “HAWZAT IMAM SWADIQ KUONGOZA MAANDAMANO YA KULAANI MAUAJI YA HUKO GAZA.”

Post a Comment

More to Read