Friday, July 4, 2014

KIKOSI MAALUM KUCHUNGUZA KIFO CHA BALOZI.



Siku mbili baada ya Kaimu Balozi wa Libya, Ismail Nwairat kujiua kwa risasi akiwa ofisini kwake, Jeshi la Polisi kupitia kikosi maalum cha uchunguzi wa matukio ya kujiua, limeanza uchunguzi wa kifo hicho.

Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema watafanya uchunguzi  wa kisayansi  kwa kutumia maofisa maalum licha ya taarifa za awali kuonyesha kuwa amejiua kwa risasi.

“Hatuchunguzi kifo pekee kwa juu juu tu, hata kama imethibitishwa amejiua ni lazima tuchunguze kwa nini amejiua, kwa mfano anaweza kuwa alitishiwa kuuawa au ana matatizo ya kifamilia, ndiyo maana akajiua au mambo mengine,” amesema.
Alisema ubalozi wa Libya umesharuhusu polisi kufanya uchunguzi ambao utashirikisha kikosi maalumu na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambao watatoa ripoti ya kidaktari ya uchunguzi wa kifo na maofisa wa ubalozi wenyewe.

“Ni lazima tupate ruhusa ya kufanya uchunguzi kutoka Ubalozi wa Libya kwa sababu kisheria masuala ya ubalozini ni ardhi ya Libya na polisi hawawezi kujichukulia uamuzi hadi tupate baraka kwanza kutoka kwa ubalozi huo,”

Kova alisema kuwa ripoti ya matokeo ya kifo hicho itatolewa baada ya muda mfupi kwani polisi hawawezi kuchukua muda katika suala nyeti kama hilo la mwanadiplomasia kujiua katika ardhi ya Tanzania.

Akifafanua namna kifo hicho kilivyotokea,  Kova amesema balozi huyo  mwenye umri wa miaka 39, alijifungia  ndani ya ofisi yake majira ya saa saba mchana na kujipiga risasi ambayo 
ilisikika hadi nje na kusababisha maafisa wa ubalozi kukimbilia kufahamu kulikoni.

Walipofika walikuta mlango umefungwa kwa ndani, walivunja na kumkuta balozi akiwa katika maumivu makali huku damu ikimminika kifuani,” amesema.
Kova aliongeza kuwa maofisa hao walimpelekaa katika hospitali ya AMI Oysterbay ambako alifariki dakika chache baadaye.

0 Responses to “KIKOSI MAALUM KUCHUNGUZA KIFO CHA BALOZI.”

Post a Comment

More to Read