Thursday, July 10, 2014

SITTA ATEUA MASHEIKH,MAASKOFU KUWAREJESHA UKAWA BUNGENI.





Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ameanza mkakati mpya wa kunusuru mchakato wa Katiba Mpya kwa kuitisha kikao cha wajumbe 27 wa Kamati ya Mashauriano ili kuondoa mpasuko kati ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wajumbe wengine.

Katika wajumbe hao wamo maaskofu wawili na masheikh wawili ambao Sitta amewateua kutoka katika Bunge la Katiba.
Sitta ameitisha kikao hicho jijini Dar es Salaam Julai 24 wakati kukiwa na matamko tofauti kuhusu mustakabali wa katiba hiyo, mengi yakieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyeshikilia hatima ya mchakato na wapinzani wakisema mkuu huyo wa nchi ndiye aliyesababisha suala hilo kwenda mrama.

Pia, Sitta ameitisha kikao hicho wakati viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakieleza kuwa suala la serikali mbili kwenye muundo wa Muungano, ambalo liligawanya wajumbe, ndiyo msimamo wa chama na wapinzani wakisema suala hilo halimo kwenye Rasimu ya Katiba na ndiyo sharti lao la kurejea bungeni.

Akizungumza  jana katika mahojiano na gazeti hili, Sitta alisema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja kutazama mwenendo wa majadiliano katika Bunge hilo na sura 15 za katiba ili kujua yapi muhimu yanayotakiwa kupewa kipaumbele kabla ya Bunge la Katiba kuanza tena vikao vyake Agosti 5.

“Sisi tumeshapeleka barua kwa wajumbe, tumehakikisha zimekwenda na katika mkutano huo tutaelewana kuhusu masuala hayo na mengine. Wasiotaka kuhudhuria wananchi watawaelewa na wataamua iwapo nia ni kususa pekee au wenzetu wana ajenda ya siri,” alisema Sitta.

Alisema katika mkutano huo, kutakuwa na utaratibu maalumu ambao utahusisha viongozi wa dini walio ndani ya Bunge kutoka madhehebu tofauti na baadhi ya wajumbe wengine kutoka kada tofauti ndani ya Bunge hilo.

“Kutakuwa na watu karibu 27, mimi nikiwa mwenyekiti. Atakayevimba kichwa na kudharau, wananchi watajua kuwa nia yake ni tofauti na katiba,”

Sitta alisema tatizo kubwa katika Bunge hilo litakalosababishwa na kutokuwapo kwa Ukawa ni  namna ya upigaji kura, lakini iwapo theluthi mbili ya wajumbe itatimia basi watakwenda  kwa mwenendo huo.

“Yapo mambo muhimu zaidi katika rasimu hii kama vile tume huru ya uchaguzi, orodha ya haki za binadamu, uongozi wa asilimia 50 kwa 50 kijinsia na kuwapa Zanzibar nafasi zaidi katika Serikali ya Muungano, mambo ambayo ni makubwa kuliko muundo...ya nini kuyapiga teke yote haya na kujikita katika muundo pekee,” alihoji.

Sitta ambaye pia alipingwa kwa kumpanga Rais Kikwete kuhutubia Bunge hilo baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba tofauti na kanuni, alisema kuwa kuususia mkutano huo wa Bunge katika kipindi chote hicho siyo hasara kwa CCM, bali kwa wananchi kwa kuwa nia ni kupata katiba bora na wala siyo kukomoana.

“Iwapo Ukawa watasusia kila kitu, basi wataonyesha kuwa siyo wakomavu wa kisiasa,” alisema mbunge huyo wa Jimbo la Urambo Mashariki.

0 Responses to “SITTA ATEUA MASHEIKH,MAASKOFU KUWAREJESHA UKAWA BUNGENI.”

Post a Comment

More to Read