Tuesday, August 26, 2014

MAMA KIKWETE AWATAKA WATANZANIA KUJENGA TABIA YA KUFANYA MAOMBI.




Na Anna Nkinda- Maelezo
26/8/2014 Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete amewataka Watanzania kujenga tabia ya kufanya maombi ili waweze kuwa karibu na Mwenyezi Mungu na kupata faraja pale wanapokabiliana na matatizo mbalimbali wanayokutana nayo katika maisha yao.
Mama Kikwete aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa mazishi ya mtoto wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Vedastus Kitwaga yaliyofanyika katika kijiji cha Usagara wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kila nafsi hai ni lazima itaonja mauti na hakuna mtu anayejua siku yake ya kufa hivyo basi ni lazima watu wajenge tabia ya kufanya ibada ili waweze kuwa karibu na Mwenyezi Mungu.

“Ukiwa na tabia ya kufanya maombi ni rahisi kwako kupata faraja hasa pale unapokutana na mambo mazito katika maisha yako  hii ikiwa ni pamoja na kuondokewa na wapendwa wako kwani maombi ni majibu ya kila jambo”, alisema Mama Kikwete.

Akihubiri katika Misa hiyo ya mazishi, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohana Mwinjili Padri John Somers aliwataka watu waliohudhuria mazishi hayo kuiga mfano wa marehemu ambaye kwa umri wake mdogo alionyesha upendo kwa jamii iliyomzunguka kwani  alikuwa kiongozi wa kanisa hii ikiwa ni pamoja na mlezi wa Umoja wa Vijana wa Kanisa la Katoliki (VIWAWA) na Katibu wa Jumuia.

“Kabla ya mauti kumkuta Marehemu alikuwa amelala nyumbani kwao Usagara tarehe 16/8/2014 ndipo akapigiwa simu na rafiki yake aliyepata ajali eneo la Tanesco Mwanza Mjini , aliamka na kwenda kutoa msaada akiwa amesimama pembeni mwa barabara akitoa huduma na wenzake ndipo gari lingine lilikosea njia na kuwagonga na hatimaye kupelekea kifo chake. Alikuwa tayari pale alipoitwa na kwenda kutoa msaada”, alisema Padri  Somers.
Akiongea kwa Niaba ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza Mhashamu Yuda Thadei Padre Robert Kitambo aliwataka wanasiasa waliohudhuria mazishi hayo kutokumsahau Mwenyezi Mungu katika maisha yao na kutosahau kuwakimbilia  watu wenye shida na kuwasaidia.

Padre Kitambo alisema kutokana na kazi nyingi za wanasiasa wengi wao wanakosa hata muda wa kuhudhuria ibada lakinijambo la muhimu ni  kumkumbuka Mwenyezi Mungu wakati uko hai.
Nawaomba muwe watetezi imara wa amani, haki, upendo na mshikamano. Angalieni leo hii tumekusanyika pamoja kwa upendo katika ibada hii ya kumuaga kijana wetu Vedastus huku kila mtu akiwa na imani yake  lakini chokochoko za dini na siasa zinatoka wapi?”, aliuliza Padre Kitambo.
Alimalizia kwa kuwataka watanzania kutumia vyombo vya moto kwa uangalifu na kufauta sheria za usalama barabani kwa kufanya hivyo ajali zitapungua na watu wengi hawatapoteza maisha kutokana na ajali hizo.

Marehemu Vedastus Kitwanga alizaliwa  tarehe 25/05/1985 na kupata elimu yake ya msingi katika shule za Usagara na Muhimbili, elimu ya Sekondari mwaka 2007 katika shule za Maua Seminari, St. Gaspar Msolwa na Mzumbe, ambapo mwaka 2010 alihitimu shahada yake ya   Bishara na kuajiriwa na Mfuko wa Pensheni wa PSPF mwaka 2012.

0 Responses to “MAMA KIKWETE AWATAKA WATANZANIA KUJENGA TABIA YA KUFANYA MAOMBI.”

Post a Comment

More to Read