Monday, September 8, 2014
BENKI KUU YA TANZANIA IMETOA RASMI TOLEO JIPYA LA SARAFU YA SHILINGI 500.
Do you like this story?
BENKI
Kuu ya Tanzania imetoa toleo jipya la sarafu ya shilingi 500 itakayoanza
kutumika Oktoba 2014 itakayokuwa mbadala wa Noti ya shilingi 500 inayoonekana
kuchakaa haraka.
Hayo yamesemwa Jijini
Dar es salaam na Mkurugenzi wa Huduma za kibenki wa benki hiyo Bw. Emmanuel
Boaz wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
“Noti ya shilingi 500
hupita kwenye mikono ya watu wengi zidi na ndiyo inayotumika zaidi kwenye
manunuzi ya kawaida hivyo kuchakaa haraka ndio maana tumeamua kutoa toleo la
sarafu itakayoanza kutumika mapema mwezi wa 10 mwaka huu.”alisema Boaz.
Akifafanua zaidi Boaz
amesema Sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi zaidi kuliko noti na pia
noti zimekuwa zilikaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye
mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe.
Akitaja sifa za
sarafu hiyo mpya Boaz amesema kwanza umbo lake ni la duara lenye michirizi
pembezoni na kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5.
Sifa nyingineni kuwa
ina rangi ya fedha na imetengenezwa kwa madini aina ya chuma na Nickel na kwa
upande wa mbele ina sura ya Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
Sheikh Abeid Aman Karume na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa
mbugani.
Pia Boaz alibainisha
kuwa sarafu hiyo kwa upande wa nyuma ina kivuli kilichojificha ambacho huonesha
thamani ya sarafu ya 500 au neno BOT inapogeuzwa geuzwa.
Kwa upande wa
matumizi Boaz amesema sarafu hiyo itakapoanza kutumika itatumika sambamba na
noti za shilingi 500 hadi zitakapokwisha kwenye mzunguko.
Benki Kuu ya Tanzania
ndiyo chombo chenye jukumu la kutoa sarafu na noti halali (legal tender)
zinazotumika nchini ambapo katika kutimiza jukumu hili Benki kuu hutengeneza
noti na sarafu zenye uwiano mzuri wa thamani (denomination) unaozingatia
uwezekano wa zile zenye thamani kubwa kuweza kugawika katika zile zenye thamani
ndogo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BENKI KUU YA TANZANIA IMETOA RASMI TOLEO JIPYA LA SARAFU YA SHILINGI 500.”
Post a Comment