Monday, September 8, 2014

YANGA, AZAM IMEKULA KWENU




KOCHA Patrick Phiri ameangalia uwezo wa Emmanuel Okwi na Paul Kiongera akawaambia Yanga na Azam akisema: “Kwa muziki huu imekula kwenu aisee.”
Mzambia  huyo anayeaminika zaidi miongoni mwa mashabiki na wanachama wa Simba, amesisitiza kwamba kombinesheni ya mafowadi hao ni matata sana na wana sifa ambazo zitawaziba midomo wale waliokuwa wakiibeza Simba.

Mashabiki wa Yanga na Azam wamekuwa wakiibeza Simba kwa madai kwamba imesajili kikosi cha kawaida ingawa kipigo cha mabao 3-0 ilichotoa kwa mabingwa wa soka wa Kenya,  Gor Mahia,  juzi Jumamosi kimewafanya watikise vichwa kwa kukubali hasa makali ya Kiongera na kumzomea Okwi.

Okwi ana utata na Yanga baada ya kusaini Simba huku akiwa na mkataba nao jambo ambalo mpaka jana Jumapili jioni lilikuwa likiwaumiza vichwa vigogo wa TFF ambao walikuwa na kikao cha kufanya uamuzi kwenye hoteli ya Colesseum jijini Dar es Salaam.

Phiri ambaye si mzungumzaji sana alisema uzuri wa Okwi na Kiongera ni kuwa wanaweza kufunga, kutafuta mipira na kupandisha mashambulizi jambo ambalo linaongeza kasi katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

“Ni jambo zuri kuwa na wachezaji wawili mbele ambao wanaweza kucheza na mpira, wanajua kufunga lakini pia ni wazuri katika kupandisha mashambulizi, hii inaongeza ufanisi wa safu ya ushambuliaji,” alisema.
“Uwezo waliouonyesha Kiongera na Okwi kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi ni wa kuvutia, wanacheza kwa kubadilika na kwa mawasiliano mazuri kwa wakati wote, hata mabao wanayofunga yanatokana na kasi yao.”

Phiri alipagawa zaidi baada ya kukumbuka ana majembe yake mengine kwenye timu za Taifa ambayo yakiripoti itakuwa ni noma zaidi.

Majembe ya Simba yaliyoko timu za Taifa ni Pierre Kwizera na Amissi Tambwe walioko Burundi pamoja na Haroun Chanongo na Amri Kiemba wa Taifa Stars. Bosi huyo amewaambia mashabiki wa Simba kwamba wasiwe na presha timu yao imerudi kwenye fomu na watafanya kitu cha ajabu ambacho pengine walikuwa hawadhaniwi kabisa wala kupewa nafasi.

Kwa upande wake Kiongera aliwatuliza mashabiki wa Simba na kuwaambia kuwa mambo mazuri zaidi yanakuja. Juzi Jumamosi mbele ya Gor Mahia,  Kiongera aliifungia Simba mabao mawili kati ya matatu ambapo moja lilifungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’, mechi hiyo ilichezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kiongera aliliambia Mwanaspoti akisema: “Huwa nafurahi sana ninapofunga lakini kufunga hakutatokea katika kila mechi, inategemea na kocha amepangaje kikosi chake.
“Ila napenda kuwaambia mashabiki wa Simba kuwa watarajie mambo mazuri kwani wachezaji wote wapo vizuri.”
Straika wa Gor Mahia Mganda, Danny Sserunkuma alisema: “Lakini Kiongera, Okwi na Owino ni wachezaji bora katika timu ya Simba kwa sababu nawafahamu na ni wachezaji ambao viwango vyao bado havijashuka kabisa.
“Kurudi kwa Okwi katika timu yake ya zamani Simba kutawasaidia sana kwani ni mtaalamu wa kutengeneza mabao na hasa wakikutana na Kiongera Simba itapata mabao mengi zaidi.”

Chanzo: Mwanaspoti

0 Responses to “YANGA, AZAM IMEKULA KWENU”

Post a Comment

More to Read